1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa Katoliki DRC lakosoa kalenda ya uchaguzi

Saleh Mwanamilongo22 Novemba 2017

Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekosoa kutangazwa kwa kalenda ya uchaguzi pasina maridhiano ya pande zote husika.

https://p.dw.com/p/2o2n0
DR Kongo Präsident Kabila einigt sich mit Opposition
Picha: Getty Images/AFP/J. D. Kannah

Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekosoa kutangazwa kwa kalenda ya uchaguzi pasina maridhiano ya pande zote husika. Msimamo huu wa kanisa unakuja wakati Waziri Mkuu wa nchi hiyo akiwasilisha bungeni sheria mpya ya uchaguzi ambayo inataka kufanya mageuzi kwenye mfumo wa uchaguzi licha ya mapungufu makubwa yanayolalamikiwa na wakosoaji wa serikali.

Kwenye ripoti yake kuhusu utaratibu wa uchaguzi nchini Kongo, Tume ya Sheria na Amani ya Kanisa Katoliki imeelezea kasoro kadhaa katika operesheni ya kuandikisha wapigakura, licha ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, CENI, kusema kuwa uandikishaji unaendelea vyema.

Ripoti ya uchunguzi wa tume ya kanisa Katoliki

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi DRC Corneille Nangaa
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi DRC Corneille NangaaPicha: Getty Images/AFP/J. Wessel

Tume hiyo ya Kanisa ambayo imefanya uchunguzi wake yenyewe, inasema kwamba kumekuweko na watu waliojiandikisha zaidi ya mara moja kwenye daftari ya wapigakura, ingawa haikuelezea ikiwa hali hiyo itaathiri vipi utaratibu mzima wa uchaguzi. Ripoti inaelezea pia kwamba kuna wapigakura walioandikishwa kwenye daftari pasina kuonesha vitambulisho vya uraia wao na kusababisha mara nyingine kuorodheshwa kwa watoto.

Padre Donatien Nshole, Katibu Mkuu wa Kongamano la Maaskofu wa Kongo, CENCO, ameserma kwamba machafuko yaliyotokea jimboni Kassai si sababu ya kuahirishwa kwa utaratibu wa uchaguzi kwenye maeneo mengine ya nchi:  "Daftari hilo ya wapigakura lina pia idadi kubwa ya watu ambao tayari wamefariki, watu waliobadili makaazi yao na kuhamia miji mingine na ambao watakuwa na tatizo la kupiga kura. Kasoro nyingine pia ni kutoorodheshwa kwa watu walioko magerezani na ambao wakati wa uchaguzi watakuwa hawana kadi za kupigia kura."

Kanisa Katoliki linaelezea pia kusikitishwa kwake na kutokuweko na kalenda ya uchaguzi iliyoafikiwa na pande zote.

Mjadala kuhusu tarehe ya uchaguzi

Hata hivyo, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi, Corneille Nangaa, ambaye alihudhuria sherehe ya kutangazwa kwa ripoti hiyo ya Kanisa Katoliki, amesema mjadala kuhusu tarehe ya uchaguzi umepitwa na wakati: "Mabishano, mijadala kuhusu kwa nini uchaguzi umeitishwa Desemba, kwa nini tarehe 23? Ni mjadala uliopitwa na wakati. Kwa wale wanaodhani kwamba tutarejelea mjadala kuhusu tarehe ya uchaguzi, wafahamu kwamba wamechelewa. Kutangazwa kwa kalenda ya uchaguzi ni mamlaka ya tume huru ya uchaguzi."

Kwa mujibu wa tume ya uchaguzi, kufikia sasa watu zaidi ya milioni 44 wameshaandikishwa kwenye daftari la wapigakura, zoezi linalotarajiwa kukamilika Januari 31 mwakani kwenye majimbo ya Kassai.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu Bruno Tshibala amewasilisha bungeni sheria mpya ya uchaguzi, sheria hiyo itakayojadiliwa mwanzoni mwa wiki ijayo, inafanyiwa mageuzi kadhaa ukilinganisha na sheria ya hivi sasa. Na huenda kukawa mgawanyo wa viti bungeni kwa mujibu wa kura kinachopata kila chama, badala ya kura za moja kwa moja kwa mgombea.

Mwandishi: Saleh Mwanamilongo/DW Kinshasa
Mhariri: Mohammed Khelef