Kanga: kito cha utamaduni wa Afrika Mashariki
Kanga za Afrika Mashariki ni mavazi maarufu yanayoonyesha kwa fahari utamaduni wa Kiswahili. Ujumbe wa kanga huwa na maana nzito na michoro ya kisasa inayovutia watu duniani kote.
Mtindo wa kihistoria
Asili ya kanga ni pwani ya Afrika Mashariki katikati mwa karne ya 19. Inaaminiwa wanawake maridadi wa Zanzibar walikuja na wazo la kuunganisha vitambaa sita vidogo vya kufunika nywele. Vitambaa hivi vilishonwa pamoja na kutengenezwa kitu kilichoitwa 'Leso' jina la vitambaa vya mraba ambavyo hapo awali vililetwa Afrika na wafanyabiashara wa Ureno. Baade likaja wazo la kutengeneza jozi ya kanga.
Vazi muhimu la Afrika
Kanga ni maarufu kwa michoro yake ya rangi za kuvutia ambayo mara nyingi huakisi maisha ya kila siku ya watu wa pwani. Michoro hiyo ni ya aina nyingi. Kuna nakshi tofauti pamoja na michoro ya ndege na maua. Kwa sasa, kanga maarufu zinapatikana katika nchi tofauti za Afrika Mashariki kama vile Tanzania, Kenya, Madagascar, visiwa vya Comoro, Msmbumbiji na Mashariki mwa DRC.
Jina latokana na aina ya ndege
Wanunuzi wa awali walikuwa wakitafuta jina la kulipa vazi hilo, na wakachagua 'kanga', ndege mwenye manyoya yenye vidoto sawa na michoro ya kanga za wakati huo.
Kivutio cha kanga ni maandishi
Kanga hazijulikani tu kwa michoro yake mizuri na rangi za kuvutia, lakini pia kwa misemo na methali inayoandikwa juu yake. Misemo ya Kiswahili ilianza kuandikwa kwenye kanga mwanzoni mwa karne hii. Kwa mfano methali inayoonekana katika moja ya kanga mbili pichani inayosema "Hekima ya mzazi yapita madegree".
Kutuma ujumbe kupitia mitindo
Wazo la kujumuisha methali, jina au ujumbe wa Kiswahili, inaaminika kuwa limetokana na mfanyabiashara maarufu wa Mombasa Kaderdina Hajee Essak, anayejulikana pia kama Abdulla. Hapo awali maandishi hayo yalikuwa ni kwa Kiarabu, kabla ya kuanza kuandikwa kwaalfabeti za Kirumi.
Zawadi ya kila msimu
Kanga mara nyingi zinatolewa kama zawadi kwa wanawake au miongoni mwa wanawake. Mivao ya kanga ni zawadi maarufu na muhimu katika sherehe za harusi nchini Kenya na Tanzania. Kanga lakini zinatumika kwa mambo mengi. Wanaume na watoto wachanga pia wanavaa kanga.
Yahamasisha watu Afrika Mashariki
Kanga inatumika kama njia ya kutangaza utamaduni wa Kiswahili, kuhamasisha watu katika masuala ya kijamii na kisiasa kupitia misemo yake. Vazi ambalo lilianza wakati wa ukoloni, ambalo bado lina nafasi kubwa katika Afrika Mashariki ya kisasa.
Mageuzi katika miundo ya kisasa
Kanga inaendelea kutumika kutangaza utamaduni wa Kiswahili, kupitia historia na mila la vazi hilo. Vazi hili linatumika kama daraja ya kuunganisha mitindo ya kizamani na ya kisasa. Wabunifu wanaitumia kanga kuonyesha ustadi wao, na kulifanya vazi hili kuendelea kwenda na wakati duniani kote. Mmoja wa wasanii wakubwa Marekani wanaotumia kanga ni Beyonce.