Kandanda la mtaani linavyoinua vipaji vya vijana
29 Novemba 2007Kandanda la mtaani linalochezwa huko Amerika ya Kusini hasa nchini Paraguay, limetokea kuvutia watu wengi hasa wapenhi wa mchezo huo, hata kufikia hatua ya kuhalalishwa katika anga la kimataifa.
Tumekuwa tukiona wachezaji nyota kutoka mataifa mbalimbali duniani, lakini huenda hatufahamu vema ni wapi watu hao maarufu hutokea hadi kujikita kileleni katika mafanikio kupitia mchezo wa kandanda.
Kandanda la mtaani huko Paraguay linasemekana kuwa mchezo wenye mvuto na hisia kubwa kwa wapenzi, na sasa tayari yameanzishwa mashindano ya kinyang’anyiro cha timu za mtaani ambapo mshindi ataondoka na kikombe kwapani.
Hakika ni mashindano ya kimataifa, kwa sababu yanashirikisha timu mbalimbali kutoka mataifa tisa ya huko Kusini mwa Amerika, na timu nyingine mbili za mtaani zimealikwa kutoka Ulaya na Afrika.
Licha ya mshindi kuondoka na kikombe, kandanda hilo la mtaani lina lengo la kuonesha vipaji vya vijana, ikiwa ni njia ya kuwafikisha katika kilele cha mafanikio kwa siku za usoni.
Ni aina ya mpira unaochezwa bila kutolewa kadi yoyote iwe ya njano kwa maana ya onyo, au nyekundu inayompeleka mchezaji nje ya uwanja, lakini wachezaji wenyewe watasuluhisha tofauti zozote zitakazojitokeza uwanjani kwa msaada wa wawezeshaji kadhaa. Kwa kifupi ni kwamba kandanda hilo la mtaani halina mwamuzi.
Mkuu wa taasisi isiyokuwa ya kiserikali inayohusika na kukuza vipaji vya vijana nchini Paraguay Luis Ramirez, amenukuriwa akisema kuwa lengo la kuanzisha aina hiyo ya kandanda ni kuwafanya vijana kuwa mahiri katika soka, na kutumia kandanda la mtaani kuwa nyenzo ya kuwawezesha kupata ajira na mafanikio maishani mwao.
Cha kushangaza zaidi katika soka hili la mtaani linalochezwa huko Amerika ya Kusini, kandanda hilo pia linahusisha walau mwanamke mmoja katika kila timu iwapo dimbani, tofauti na mchezo wa soka la wanaume tuliouzoea.
Si hilo tu la kustaajabisha, kwani pia soka hili la mtaani halitoi ushindi kwa timu inayofunga magoli mengi dimbani, bali ushindi hutolewa kwa kuangalia vigezo vya nidhamu na heshima miongoni mwa wachezaji uwanjani.
Kabla ya kuanza mpambano, wachezaji kupewa maelekezo ya nidhamu wawapo uwanjani, na ikiwa timu moja itacheza mchezo mchafu, haitapata kikombe cha ushindi wala zawadi yoyote hata kama itafunga magoli mengi.
Alama hutolewa katika kipindi cha tatu, kwa kufanya majadiliano yanayoangazia kwenye uwajibikaji uwanjani, heshima mchezoni na hapo ndipo ushindi utatolewa kwa timu iliyofanikiwa kuzingatia vigezo vyote vya mchezo.
Kandanda la mtaani limepata umaarufu katika nchi za Paraguay, Argentina, Bolivia, Brasil, Colombia na Ecuador.
Nchini nyingine zinazosakata kabumbu hilo ni Peru, Chile, Uruguay Afrika Kusini na U jerumani.