Kandanda la China lawavutia wachezaji nyota
6 Februari 2016Teixera alikuwa akiwindwa sana na kalbu ya Liverpool ya England. Uhamisho huo mkubwa umekuja siku tatu pekee baada ya klabu ya Guangzhou Evergande kulipa euro milioni 42 kuipata saini ya mshambuliajii wa Atletico Madrid Jackson Martinez, na siku tisa baada ya Jiangsu kumnunua kiungo Mbrazil Ramires kutoka Chelsea kwa euro milioni 28.
Usajili wa Teixeira mwenye umri wa miaka 26 kutoka klabu ya Ukraine, Shakhar Donetsk unaonyesha kuwa China sasa ina misuli ya kuwavutia wachezaji walio katika kilele cha taaluma zao. Kocha wa Chelsea Guus Hiddink alizungumzia hilo. Alisema "Nadhani kuna umuhimu sawa kwa China, kuendeleza kandanda la China, kuwaleta watu wa tajriba kubwa wanaojua kuelimisha na namna ya kuwa na vituo vya kandanda na kadhalika. Haiwezi tu, katika maoni yangu kununua tu na fedha nyingi wachezaji nyota na kudhani kuwa umeweka msingi wa kandanda la China".
Kumekuwa na maswali kuhusu ikiwa baadhi ya uhamisho huu umekuwa ghali kupindukia, huku mikataba mingi ya msimu huu ikiwahusisha wachezaji wa kati ya miaka 27 hadi 30, ikiwa ni umri mdogo kuliko ule wa wachezaji nyota waliokuwa wakielekea mashariki kucheza kandanda katika miaka ya nyuma wakiwa na lengo la kujipa fedha wakati wakimalizia taaluma zao. Lakini alipoulizwa ikiwa hali hii inazusha wasiwasi, kocha wa Arsenal Arsene Wenger alijibu…"Ndiyo bila shaka. Wka sababu China inaonekana kuwa na nguvu za kifedha kuihamisha ligi zima ya Ulaya na kuipeleka China na sote tunajua, tumekuwa katika kazi hii kwa muda mrefu kujua kuwa hayo ni matokeo ya nguvu za kiuchumi ambazo wanazo. Je wataweza kuendeleza hamu ya kufanya hilo? kwa sababu nakumbuka miaka michache iliyopita Japan ilianza kufanya hivyo na wakapunguza mwendo baadaye. Lakini sijui hamu ya China iko vipi lakini ni hamu kubwa ya kisiasa, tunapaswa kuwa na wasiwasi".
Makampuni ya China yamewekeza kiasi kikubwa ca fedha katika kandanda tangu Rais mpenda kandanda Xi Jinping alitangaza kuwa kuandaa, kufuzu na kushinda Kombe la Dunia ni malengo ya taifa hilo.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA/Reuters
Mhariri: Josephat Charo