KANDAHAR: Jeshi la NATO lafanya operesheni dhidi ya Taliban
6 Machi 2007Majeshi yanayoongozwa na shirika la NATO nchini Afghanistan yameanza operesheni dhidi ya wanamgambo wa Taliban katika mkoa wa kusini wa Helmand nchini humo.
Operesheni hiyo inayowajumulisha wanajeshi 5,500 wa jeshi la NATO na wanajeshi wa Afghanistan, imeanza saa kumi na moja alfari ya leo.
Kamanda wa kikosi cha ISAF katika eneo hilo, Ton Van Loon, amesema operesheni hiyo kwa jina Achilles, inawajumulisha pia wanajeshi wa Afghanistan na inafanyika kufuatia ombi la serikali ya Kabul.
Aidha Loon amesema harakati hiyo inalenga biashara ya bangi na kuboresha usalama kaskazini mwa mkoa wa Helmand ambako wanamgambo wa Taliban waliyateka maeneo kadhaa mwanzoni mwa mwezi uliopita.
´Tunajua kwamba wanamgambo wa Taliban wamekuwa mara kwa mara wakitafuta hifadhi katika jamii zenu na wamewatumia wananchi waaminifu na watoto kama ngao kujilinda. Hivi ndivyo wanavyofanya na nataka kuwahakikishia kwamba tunatambua ujanja wa adui. Huku operesheni ya Achilles ikiwaleta wanajeshi zaidi wa ISAF na wa Afghanistan katika maeneo yenu, musiwe na wasiwasi. Tunawatafuta wanamgambo.´
Wakati haya yakiarifiwa, raia tisa wameuwawa kwenye shambulizi la bomu katika mkoa wa Kapisa kaskazini mwa mji mkuu Kabul.
Naibu wa gavana wa mkoa huo, Sayed Mohammad Hashimi, amesema shambulio lililofanywa na jeshi la Marekani limeyalenga makaazi ya wanamgambo wa Taliban wanaofanya mashambulizi ya maroketi dhidi ya kambi za majeshi ya muungano zilizo karibu.
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai, ameyalaani mauaji hayo ya raia na uchunguzi unafanywa na maafisa wa Marekani na Afghanistan.