Kampeni za uchaguzi wa bunge zaanza mashariki mwa Congo
20 Machi 2019Baada ya wakaazi wa miji ya Beni na Butembo na wilaya ya Beni katika mkoa wa Kivu ya kaskazini pamoja na wilaya ya Yumbi katika mkoa wa Paindombe magharibi mwa DRC kunyimwa haki yao ya kupiga kura desemba thelathini Mwaka uliopita,kutokana na homa ya Ebola pamoja na usalama mdogo, wakaazi hao watapiga kura kuwachaguwa wabunge wao machi 31.
Kampeni za uchaguzi zimeanza na wagombea ubunge wamekuwa wakipiga debe kuwatafuta wapiga kura. Katika mitaa ya Beni,Butembo pamoja na wilaya ya Beni, wagombea ubunge wa mkoa pamoja na ule wa kitaifa wamekuwa wakizunguka wakipiga debe, katika kampeini ya kutafuta wapiga kura.
Wagombea walalamika kukosa pesa
Wagombea wengi katika mitaa ya mji wa Beni wamekuwa wakilalamikia pesa walizozitumia wakati wa kampeni ya uchaguzi Desemba thelathini, kabla ya tume ya uchaguzi CENI kutangaza kuahirishwa kwa uchaguzi katika eneo hilo.
Wagombea wengi wamesema hawana pesa za kutosha kwaajili ya kufanya kampeni, na baadhi yao wameridhika kutumia nyimbo zao za kampeni kwenye radio, kuomba kura za wakaazi.
Katika uchaguzi huu kura zitapigwa kwa siri, na wagombea wengi wamekuwa wakipata ahadi za wapiga kura. Baada ya tume huru ya uchaguzi CENI kuahirisha uchaguzi, wakaazi wengi waliowahi kumiminika kwa wingi katika zoezi la kupangwa la kupiga kura hewa desemba thelathini Mwaka jana, wameonesha nia yao ya kubaki majumbani siku ya uchaguzi yaani machi 31, baada ya kukasirishwa na hatua ya Ceni ya kutowatangaza wagombea waliochaguliwa katika uchaguzi hewa Mwaka jana.
Na zikiwa zinasalia siku kumi na moja,wakaazi wa maeneo haya wapige kura,Kuna wagombea ambao bado hawajajitokeza katika harakati za kampeni.
John Kanyunyu, DW, Beni