Kampeni ya kuhamasisha wananchi kuhusu haki zao Kenya
24 Oktoba 2023Mawakili kote nchini wamejitolea kutoa hamasa kwa Wakenya kwa muda wa wiki moja. Kupitia zoezi lililopewa jina, "Wiki ya Uhamishaji wa kisheria'' mawakili wanachukua muda huu kutangamana na wananchi, kuwapa mafunzo kuhusu vipengee tata vya sheria, na kuwapa umma ushauri na usaidizi wa kisheria kuhusu masuala binafsi yanayowatatiza.
Akizindua zoezi hili, mwenyekiti wa chama cha mawakili nchini Kenya Eric Theuri ameitolea mwito serikali kuongeza idadi ya waendesha mashtaka mahakamani.
"Tufanye mazungumzo ambayo zaidi ya magereza, wahalifu na wahanga, tuzingatie mfumo ambao unaleta haki, ambao unapunguza au kuvunja tabia ya kurejelea uhalifu.”, alisema Theuri.
Dhamira ya zoezi hili ni ‘juhudi za pamoja ili kupunguza msongamano magerezani na kutoa huduma muafaka za kisheria'. Mahakama nchini imekuwa ikitilia mkazo haja ya kuungwa mkono njia m'badala za kutatua kesi ili kuzuia msongamano wa wafungwa gerezani.
''Ukaguzi wa mfumo wa haki za jinai, umeonyesha kuwa, unawanyanyasa masikini.''
Aidha mrundikano wa kesi mahakamani ambazo zinaweza kutatuliwa kwa kuwatumia wapatanishi husababisha kucheleweshwa kwa haki.
Renson Ingonga, mwendesha mashtaka mkuu wa umma nchini, ametoa wito kwa wadau kwenye sekta ya sheria kufanya kazi kwa pamoja.
"Ukaguzi wa mfumo wa haki za jinai, umeonyesha kuwa, unawanyanyasa masikini. Hili linajitokeza kutokana na tabia ya kuwabagua watu kutokana na umasikini wao, masharti ya dhamana yanayopita kiasi, na watu kukamatwa kiholela. Hili ni tatizo la kimfumo linalotuhitaji tuungane, ili kwa pamoja tuhakikishe kwamba hakuna unyanyasaji.”
Zoezi hili linajiri wakati msako wa kuwakamata watu wanaojifanya kuwa mawakili nchini ukiwa umeshika kasi. Brian Mwenda anayejiita wakili, aliyekamatwa jijini Nairobi alifunguliwa mashtaka mahakamani huku watu wengine watatu waliojifanya mawakili wakikamatwa mjini Kisii.
Grace Njeri, wakili anayehudumu mjini Nakuru anasema pia wanatumia muda huu kutoa hamasa kwa umma kuhusu namna ya kuwatambua mawakili wa uwongo.
"Hakikisha wakili amekuonyesha kitambulisho chake cha kazi. Na ukiangalia kwenye tovuti ya chama cha mawakili na kuona hakitumiki, hiyo inamaanisha wakili huyo hawezi kutoa huduma ya kisheria.”
Zoezi hili la hamasa ya kisheria litakamilika tarehe 27 mwezi huu.