1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni ya kimataifa kuitenga Urusi yaendelea

19 Machi 2014

Kampeni ya kimataifa ya kuitenga Urusi kwa msimamo wake juu ya Crimea inazidi, huku Marekani ikituma meli kwenye Bahari Nyeusi, nako Crimea bendera za Urusi zikipepea kwenye makao makuu ya jeshi la majini.

https://p.dw.com/p/1BSEi
Bendera ya Urusi ikipepea kwenye makao makuu ya jeshi la majini la Ukraine katika jimbo la Crimea.
Bendera ya Urusi ikipepea kwenye makao makuu ya jeshi la majini la Ukraine katika jimbo la Crimea.Picha: Reuters

Rais Vladimir Putin wa Urusi anakabiliwa na shinikizo kutoka kila upande, ingawa haonekani kutikisika hadi sasa panapohusika dhamira ya nchi yake kuichukua tena Crimea.

Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, amekuwa kiongozi wa hivi karibuni kabisa kupaza sauti yake juu ya hatua hiyo ya Urusi, wakati akizungumza kwenye bunge la nchi yake hivi leo, ambapo alisema anashauriana na wenzake wa kundi la mataifa tajiri duniani la G7 juu ya kukabiliana na Urusi.

"Tunalaani hatua za Urusi ambayo katika karne ya 18 iliasaini mkataba ambao uliirejesha Crimea kwa Urusi. Na tunaiona hatua hii ikivunja mamlaka na heshima ya taifa la Ukraine. Japan haitalichukulia kijuujuu jaribio lolote la kubadilisha hali iliyopo kwa kutumia nguvu." Alisema Abe.

Tayari Japan ilishatangaza tangu jana kwamba itasimamisha mazungumzo yaliyokuwa yanaendelea juu ya uwekezaji na ulegezaji wa masharti ya viza kati yake na Urusi kama sehemu ya vikwazo vyake.

Kampeni ya kimataifa dhidi ya Urusi

Marekani hivi sasa inaongoza kampeni za kimataifa kuitenga zaidi Urusi na mkutano wa mataifa ya G7 unaofanyika wiki ijayo mjini The Hague utajikita kwenye hatua hizo, kwa mujibu wa Ikulu ya Marekani.

Watu wenye silaha wanaoaminika kuwa wanajeshi wa Urusi wakilinda makao makuu ya jeshi la majini la Ukraine katika jimbo la Crimea.
Watu wenye silaha wanaoaminika kuwa wanajeshi wa Urusi wakilinda makao makuu ya jeshi la majini la Ukraine katika jimbo la Crimea.Picha: Reuters

Msimamo kama huo pia umeoneshwa na Waziri Mkuu wa Australia, Julie Bishop, ambaye ameliambia bunge hivi leo kuwa hatua ya Urusi kuichukua Crimea haikuwa halali na inapaswa kukabiliwa kwa hatua kali.

"Serikali ya Australia itaweka vikwazo kwenye sekta ya fedha na marufuku ya kusafiri kwa wale ambao wamekuwa mbele katika kitisho cha Urusi dhidi ya mamlaka ya Ukraine. Hatua zilizochukuliwa na Urusi ni uvunjaji wa wazi wa kanuni za kimataifa zinazokataza matumizi ya nguvu na kulinda heshima ya mataifa." Alisema Bishop.

Ukraine yaapa kutoondoa majeshi yake Crimea

Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Ulinzi wa Ukraine, Ihor Tenyukh, amesema nchi yake haitawaondoa wanajeshi wake kwenye mkoa wa Crimea, licha ya Rais Putin kutangaza rasmi kuwa Crimea ni sehemu ya Shirikisho la Urusi.

Ujumbe wa Crimea ukiwa kwenye jengo la bunge la Urusi, Duma.
Ujumbe wa Crimea ukiwa kwenye jengo la bunge la Urusi, Duma.Picha: Reuters

Kauli hiyo wakati bendera tatu za Urusi zikionekana kupepea kwenye makao makuu ya jeshi la majini la Ukraine kwenye bandari ya Sevastopol huko Crimea. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wanajeshi wanaokisiwa kuwa ni wa Urusi wanalinda makao makuu hayo huku pia wakiwepo wanamgambo wa "vikosi vya ulinzi", ambavyo vinaundwa na wapiganaji wanaoiunga mkono Urusi.

Tayari Waziri Mkuu wa Ukraine, Arseny Yatsenyuk, amemuamuru naibu wake wa kwanza, Vitaly Yarem, na waziri huyo wa ulinzi kwenda Crimea kujaribu kutuliza hali na "kuhakikisha kuwa mgogoro wa Crimea haugeuki kuwa wa kijeshi."

Marekani yatuma meli Bahari Nyeusi

Wakati huo huo, Marekani imetuma meli yake ya kivita kwenye mafunzo ya siku moja ya kijeshi kati yake na majeshi ya majini ya Bulgaria na Romania kwenye Bahari Nyeusi.

Meli ya kivita ya Marekani, USS Truxtun, ikiondoka Istanbul, Uturuki, kuelekea kwenye Bahari Nyeusi, kwa ajili ya kushiriki mafunzo ya kijeshi na Bulgaria na Romania.
Meli ya kivita ya Marekani, USS Truxtun, ikiondoka Istanbul, Uturuki, kuelekea kwenye Bahari Nyeusi, kwa ajili ya kushiriki mafunzo ya kijeshi na Bulgaria na Romania.Picha: Reuters

Crimea iko kwenye upande wa kaskazini wa bahari hiyo na Marekani inaiita hatua hii ya leo kuwa ni jambo la kawaida lililopangwa hata kabla ya kuanza kwa mzozo nchini Ukraine.

Hata hivyo, afisa mahusiano wa Kikosi cha Jeshi la Marekani barani Ulaya, Shawn Eklund, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa Marekani inapaswa "kuwaunga mkono washirika wake kwenye Jumuiya ya Kujihami ya NATO" katika eneo hilo.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters/AFP/AP
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman