Kamishna mkuu wa haki za Binaadamu wa Umoja wa mataifa kuizuru China
25 Agosti 2005Kinachozingatiwa na wengi panapotajwa Jamhuri ya watu wa China, ni masuala ya uchumi na haki za binaadamu. Jumatatu ijayo kamishna wa haki za binaadamu wa Umoja wa mataifa Louise Arbour ataizuru China ambako atabakia hadi tarehe 2 Septemba. Kutokana na hayo wasomi 600 wa Kichina walimuandikia barua ya wazi kamishna huyo mnamo wiki iliopita, wakikosoa vikali kutiwa nguvuni mwanaharakati wa kichina wa haki za binaadamu, kukandamizwa uhuru wa vyombo vya habari na ukosefu wa mageuzi ya kisiasa.
Muasisi wa barua hiyo ya wazi kwa kamishna wa umoja wa mataifa anayehusika na haki za binaadamu, kwa lugha ya Kiingereza na Kichina ni mpigania haki za kiraia Li Jian, ambamo sehemu kubwa inakosoa vikali juu ya hali ya haki za binaadamu nchini China. Ukilinganisha na kasi ya ukuaji uchumi ni jambo la kusikitisha. Kwa mfano kwa sababu ya utoaji maoni yao na harakati zao za kidini-wengi wamewekwa kizuizini, na mara nyingi bila ya kufikishwa mahakamani. Li Jian kwa hivyo anasema,“Tunatumai kamishna wa haki za binaadamnu awa umoja wa mataifa atazungumza kinaga ubaga na Viongozi wa serikali ya China, juu ya suala hili kulipatia suluhisho muwafaka.”
Ziara ya kamishna Arbour itafanyika katika wakati ambao China kwa upande mwengine, imekubali kwa mara ya kwanza kumruhusu mjumbe wa ngazi ya juu wa umoja wa mataifa uakiwa na kibali cha kuchunguza madai ya mateso kuizuru nchi hiyo. Manfred Nowak, mchunguzi maalum wa tume ya haki za binaadamu ya umoja wa mataifa inayohusika na masuala ya uteasaji na amaovu mengine dhidi ya binaadamu kama ni adhabu, ataizuru China kuanzia Novemba 21 hadi Desemba 2 mwaka huu, ili kuonana na maafisa wa serikali mjini Beijing na kujionea mwenyewe hali ilivyo katika magereza nchini China. Ripoti yake itajumuishwa katika ripoti atakayoiwasilisha mbele ya mkutano wa tume ya haki za binaadamu ya umoja wa mataifa mwaka ujao. Wakati China haikuwahi kutoa ruhusa ya aina hiyo mnamo miaka ya nyuma, hata hivyo iliwahi kuwaruhusu wataalamu wa masuala ya kuvumiliana kwa watu wa dini mbali mbali na utiaji watu nguvuni kiholela bila kuwafikisha mahakamani kwa sababu ya imani zao kuizuru Beijing hapo kabla.
Wasomi na waandishi vitabu mashuhuri waliosaini barua hiyo ya wazi kwa kamishna wa umoja wa mataifa ni pamoja na Mo Li ambaye binafsi alionja machungu ya ukandamizaji nchini China. Baada ya kukandamizwa kwa vuguvugu la wanafunzi kudai mabadiliko 1989, Mo aliwekwa gerezani, alipoikosoa serikali ya kikoministi iliokua madarakani awakati ule. Kwa wakati huu anaishi uhamishoni lakini akiendelea na harakati za kupigania kuheshimiwa kwa haki za binaadamu nchini China. Aeleza kuwa,“ Nilipotumiwa barua ya Li Jian niliisoma kwa shauku kubwa. Niliyaona yaliomo kuwa ni mazuri na hivyo nikaamua nami pia kuitia saini. Kamishna wa haki za binaadamu wa umoja wa mataifa Bibi Arbour ataitembelea China kwa sababu anataka kujionea hali ilivyo. Lakini utawala huu wa kidikteta wa chama cha Kikoministi una desturi ya kuficha ukweli. Unataka tu kuonyesha upande ulio mzuri . Hivyo hapa kuna umuhimu mkubawa wa kusikiliza maoni ya wananchi wenyewe.”
Muasisi wa barua hiyo Li Jian ,kuwepo kwa hali mbaya ya haki za binaadamu nchini China kunachangiwa na haya yafuatayo:- Urasimu, rushwa na uchujaji na utupiaji jicho kutoka kwa maafisa wa chama tawala cha Kikoministi. Kwa hivyo Li anamatumaini kuwa,“Kwanza tunatumai kuwa tume ya haki za binaadamu ya umoja wa mataifa itaitaka serikali ya China kuboresha hali ya haki za binaadamu nchini. Na pili tunataka sisi kama wanaharakati wa kupigania haki za kiraia tushirikishwe katika mazungumzo na tume hiyo ya umoja wa mataifa.”
Wakati wa ziara hiyo nchini China , kamishna wa haki za binaadamu wa umoja wa mataifa Bibi Arbour atahudhuria pia warsha ya 13 ya haki za binaadamu katika kanda ya Asia na Pacific.