1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi ya jeshi yashambuliwa Venezuela

Sylvia Mwehozi
7 Agosti 2017

Jeshi la Venezuela linaendelea na msako mkali dhidi ya askari mamluki ambao walikimbia na silaha baada ya kushambulia kambi ya kijeshi katika kile walichokiita ni kuupinga "udhalimu wa mauaji " wa Rais Nicolas Maduro. 

https://p.dw.com/p/2hoIQ
Venezuela Krise - Präsident Maduro während seiner TV-Ansprache
Picha: Reuters/Miraflores Palace

 

Maafisa wamesema mashambulizi hayo yalifanywa na wapiaganaji wapatao 20 wakiongozwa na afisa wa jeshi ambaye alikimbia vikosi vinavyopambana katika kambi hiyo kwenye mji wa tatu kwa ukubwa, Valencia, kwa muda wa masaa matatu mapema hapo jana.

Mashambulizi hayo yalimalizika baada ya washambuliaji wawili kuuliwa na wengine wanane kukamatwa, amesema Rais Nicolas Maduro kupitia televisheni. Wengine 10 walitoroka na bunduki ambazo walizichukua kutoka katika kambi hiyo, kwa mujibu wa afisa mmoja ambaye anadai msako mkali bado unaendelea.

Venezuela Krise - Straßenproteste
Wanaharakati wanaopinga serikali wakiweka vizuizi barabarani mjini ValenciaPicha: Getty Images/AFP/R. Schemidt

Rais Maduro amelaani mashambulizi hayo akisema ni "mashambulizi ya kigaidi dhidi ya vikosi vya kijeshi". Maduro anadai kwamba wale wanaodaiwa kuhusika wanafadhiliwa na fedha kutoka Marekani na Colombia, na kuwaita "mamluki na magaidi". Maduro amesema kwamba "mashitaka tayari yamepangwa na nimeomba kifungo cha juu zaidi kwa wale wote waliohusika katika mashambulizi haya ya kigaidi, kifungo cha juu na hakuna mafao kwa ndugu au wale walioasi."

Vuguvugu hilo ambalo limeripotiwa kama "Operesheni David" linamlenga moja kwa moja rais huyo anayepingwa. Venezuela imetumbukia katika mgogoro mkubwa wa kisiasa wakati Maduro akielekea kujipatia mamlaka zaidi baada ya miezi kadhaa ya maandamano na vurugu dhidi ya utawala wake.

Mmoja wa viongozi wa mashambulizi hayo, Kapteni Juan Carlos Caguaripano, amenukuliwa na tovuti ya El Nacional akisema kwamba njama hizo zililenga kukabiliana na mipango ya kuibadili katiba. Caguaripano alijificha mwaka 2014 baada ya kutangaza uasi dhidi ya Maduro na kuondolewa kutoka jeshini. "Tunajitangaza wenyewe kuwa ni waasi halali, tumeungana kwa umoja na watu wenye ujasiri wa Venezeuela, kukataa uonevu wa mauaji ya Nicolas Maduro," amesema Juan. 

Venezuela Gerneralstaatsanwältin Luisa Ortega Diaz in Caracas
Aliyekuwa mwanasheria mkuu wa Venezuela Luisa Ortega DiazPicha: picture-alliance/dpa/W. Riera

Kufuatia kura ya hivi karibuni iliyoamuriwa na Maduro na kulaaniwa na jumuiya za kimataifa kama yenye kutaka kujiogezea madaraka, serikali ya Venezuela ilijipatia viti 545 vya bunge maalumu ambalo litapewa kazi rasmi ya kuandika upya katiba.

Likiwa upande wa Maduro, bunge hilo litakuwa na mamlaka ya kuvunja bunge la sasa linalodhibitiwa na upinzani. Katika hatua za awali zilizokwishachukuliwa na chombo hicho, bunge la katiba tayari limemfuta kazi Mwanasheria Mkuu Luisa Ortega Diaz siku ya Jumamosi. Ortega ni mkosoaji mkubwa wa Rais Maduro.

Licha ya kuwa na hazina ya utajiri mkubwa wa mafuta taifa hilo linakabiliwa na mfumuko wa bei na uhaba mkubwa wa vyakula, madawa na bidhaa nyingine muhimu.

Mwandishi: Sylvia Mwehozi/AFP/dpa

Mhariri: Mohammed Khelef