Kambi ya Dadaab yakabiliwa na mgogoro wa kibinaadamu
12 Julai 2012Kundi la mashirika nane ya misaada yakiwemo CARE, International Rescue Committee, Oxfam na Save the Children limesema fedha kwa ajili ya huduma muhimu zitaisha ndani ya miezi miwili au mitatu, hali inayowaweka maelfu ya wakimbizi katika kambi hii, ambayo tayari inakabiliwa na hali isiyotabirika ya usalama, katika hatari.
Katika taarifa yao ya pamoja waliyoitoa siku ya Alhamis, mashirika hayo yamesema, yanahitaji kiasi cha dola za Marekani milioni 25 kuendela kuwahudumia wakimbizi siyo chini ya laki mbili wanaokimbia vita na njaa nchini Somali. Yamesema kupungua kwa ufadhili kunatishia afya, usalama na maisha kwa ujumla, na kuongeza kuwa kambi hiyo ya Dadaab ilikua kwa zaidi ya theluthi moja mwaka uliyopita kufuatia kuingia kwa mkupuo, Wasomali 160,000 nchini Kenya.
Afisa habari na mawasiliano wa shirika la Oxfam nchini Kenya Alun McDonald hali kambini hapo ni ya dharura na kwamba uwezo wake haukidhi mahitaji ya sasa. "Kiasi cha pesa kilichopo sasa hivi hakitoshi kukidhi mahitaji ya wakimbizi wanaozidi kuongezeka na kuna karibu watu nusu milioni katika kambi hii. Kwa hivyo katika miezi michache ijayo, huduma muhimu kama vile maji, afya na elimu zitasimishwa au kupunguzwa kwa kiasi kikubwa," ameiambia DW katika mahojiano maalumu.
Ukame watishia tena Somalia kusini
Wakati wasomali hao waliingia Kenya wakikimbia vurugu, ukame uliokithiri na njaa vilivyoikumba Somalia mwaka uliyopita, mashirika ya misaada yameonya kuwa eneo la kusini mwa Somalia linaweza kutumbukia tena katika janga la njaa kufuatia mvua zisizoridhisha na vita vinavyoendelea. Alun ameitaka jumuiya ya kimataifa kuendelea kusaidiana na serikali ya Kenya kuhakikisha kambi hiyo inaendelea kuwahudumia wakimbizi.
"Serikali ya kenya imebeba jukumu zito kwa kuwapokea wakimbizi nusu milioni katika mpaka wake na jumuiya ya kimataifa inapaswa kuendeleza msaada kwa kambi ya Dadaab," alisema, na kuongeza kuwa ipo haja kwa jumuiya ya kimataifa kuanzisha mjadala juu ya ukomeshaji wa vita nchini Somalia. Alisema wakimbizi wengi katika kambi ya Dadaab wanapenda kurejea makwao lakini kwa sasa hivi hawezi kufanya hivyo na kwamba suluhisho la Dadaab linaweza kupatikana tu kupitia Somalia yenye amani.
Hali ya usalama katika kambi hiyo inatia mashaka na inafanya shughuli za wafanyakazi wa mashirika ya misaada kuwa ngumu. Mwezi uliyopita, watu wenye silaha wa liwateka wafanyakazi wanne katika kambi hiyo, katika moja ya matukio ya hivi karibuni ya utekaji nyara na mashambulizi ya mabomu. Wafanyakazi hao walikuja kuokolewa baadaye, lakini wengine walioteka kutoka kambini hapo wanaendelea kushikiliwa mateka nchini Somalia.
Thelathini elfu hawana mahema ya kulalia
Taarifa imesema mahema yanahitajika kwa ajili ya watu 30,000, lakini mashirika hayo yana uwezo kwa ajili ya watu elfu nne tu. Wanawake na watoto wako katika hatari ya kubakwa kutokana na kutembea umbali mrefu kutafuta kuni au kutembea kwenya maliwati. taarifa hiyo inasema vitendo vya unyanyasaji wa ngono vimeongezeka kwa asilimia 36.
Kambi ya Dadaab iliundwa miaka 20 iliyopita na imekuwa ikipanuka kadiri wakimbizi wanavyozidi. Jambo hili limefanya mahitaji ya kambi hiyo kuongeza kwa kiasi kikubwa, yamesema mashirika hayo, ambayo pia yanahusisha Catholic Relief Services, Danish Refugee Council, Lutheran World Federation na Terre des Hommes.
Yameonya kuwa kupunguza misaada kwa kambi hiyo, kunaweza kuharibu zaidi hali ya usalama, na kwamba endapo watoto hawatokwenda shule, na watu wakakosa makaazi sahihi na huduma nyingine, hii inaweza kuchochea vitendo vya kijeshi, vurugu na kukosekana kwa utulivu.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman