Kamati ya Kimahakama yapiga kura kuhusu Kavanaugh
28 Septemba 2018Shughuli hiyo ya upigaji kura inajiri wakati ambapo Chama cha Wanasheria cha Marekani kikiiomba Kamati ya Kimahakama na baraza zima la Seneti kutoharakisha shughuli ya upigaji kura kuhusu Kavanaugh, kwa nafasi ya Mahakama ya Juu hadi Idara ya Ujasusi ya Marekani itakapofanya uchunguzi kamili wa madai yaliyoibuliwa dhidi yake.
Upigaji kura wa awali unaonesha katika kamati hiyo ya Seneti unaonesha kuwa kura zimegawanyika kwa kura 11 na 10 ambapo wengi ni wa chama cha Republican. Wanachama wa Democrats wanatarajiwa kupinga uteuzi huo. Kati ya wanachama kumi na moja wa Republican walioko katika Kamati ya Kimahakama, ni kura moja tu ya Seneta Jeff Flake wa Arizona ambayo inatiliwa shaka. Katika kikao cha Seneti cha kusikiliza maelezo yaliyotolewa na Christine Ford na Bett Kavanaugh jana, wawili hao walisema kisa hicho kinachodaiwa kutokea miaka 36 iliyopita kimeathiri maisha yao kwa njia moja au nyingine.
Ford alisema kwamba alifika mbele ya Seneti kwa kuwa alitaka mwenyewe na kwamba anaamini ni jukumu lake la kiraia. Aliilezea Seneti kuhusu alivyomfahamu Kavanaugh na kusema kwamba mwaka 1982 alihudhuria sherehe katika nyumba ya Kavanaugh. Hata hivyo alisema hakumbuki maelezo yote kuhusu jinsi sherehe hizo zilipangwa, na kwamba yaliyomfikisha mbele ya bunge hilo hawezi kulisahau. "Nilisukumwa kitandani na Brett aliruka juu yangu. Alianza kunipapasa. Nilijaribu kupiga kelele nikiwa na imani kuna mtu atanisikia. Nilijaribu kutoroka lakini alikuwa mzito. Alijaribu kunivua nguo. Niliamini alitaka kunibaka. Nikaendelea kupiga kelele tena lakini Brett akanifunga mdomo kwa mikono yake. Hapo nilikuwa na wasiwasi kwamba angeniua bila kukusudia. Hiki ndicho kitu ambacho kimekuwa na athari kubwa katika maisha yangu."
Kavanaugh akanusha madai ya unyanyasaji wa kingono
Kwa upande wake, Kavanaugh alisema kwamba sherehe ambako kisa hicho kinadaiwa kutendeka huenda zilifanyika wakati wa wikendi. Anasema kalenda yake inaonesha kwamba alikuwa mjini Washington kwa wikendi moja ambayo ni Juni tarehe 4 mwaka 1982, na kwamba siku hiyo alikuwa na baba yake katika mashindano ya gofu. Aidha anasema kwamba anaweza kushindwa katika upigaji kura lakini hatua hiyo haiwezi kamwe kumfanya kuiachia azma yake: "Munaweza kunishinda katika kura ya mwisho, lakini hamuwezi kunifanya kuiacha nia yangu. Niko hapa leo kusema ukweli. Sijawahi kumdhulumu yeyote kingono. Si katika shule ya sekondari, wala chuo, wala siku yoyote ile. Unyanyasaji wa kingono ni jambo la kutisha."
Licha ya kuwa Seneti inatathmini iwapo itapendekeza Kavanaugh kuidhinishwa, Bunge lote la Seneti huenda likaanza kupiga kura ya utaratibu kesho Jumamosi, na kuweka kura ya mwisho Jumanne wiki ijayo.
Mwandishi: Sophia Chinyezi/APE
Mhariri: Mohammed Khelef