1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamata kamata yaanza Kenya

31 Januari 2018

Kamata kamata huko Kenya imeanza kushuhudiwa baada ya kiongozi wa upinzani nchini humo Raila Odinga kujiapisha kama rais wa wananchi hapo Jumanne.

https://p.dw.com/p/2rqio
Kenia "Vereidigung" von Raila Odinga in Uhuru Park in Nairobi
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Wakili Tom Kajwang aliyesimamia hatua hiyo ya kujiapisha Raila Odinga ametiwa nguvuni huku Serikali ikisema kuwa watu wengi watakamatwa. Wakati huo huo serikali imesema wakenya wataendelea kukosa kutizama vituo vitatu vya televisheni hadi uchunguzi utakapokamilika.

Siku moja baada ya Raila Odinga kujiapisha kuwa rais wa wananchi wa Kenya serikali imemkamata wakili Tom Kajwang aliyesimamia kiapo cha Odinga. Hata hivyo hapajatolewa taarifa zozote kuhusu sababu za kumtia nguvuni.

Wakili huyo ambaye ni mwanachama wa Muungano wa NASA alikamatwa na maafisa wa ujasusi alipokuwa mahakamani. Waziri wa usalama Fred Matiang'i aliyetaja hafla hiyo kuwa kinyume cha sheria amesema uchunguzi unaendelea na kuwa watu kadhaa watatiwa nguvuni.

Vituo vya televisheni vitazimwa hadi uchunguzi ukamilike

Waziri Matiangi amedokeza kuwa sasa wanavichunguza vituo vya televisheni vya KTN, Nation Media Group pamoja na Citizen ambavyo amevitaja kuwa huenda vilikuwa na nia ya kushirikiana na wahalifu.

Fred Matiangi vorne links
Waziri wa usalama wa ndani Kenya, Fred Matiang'i (kushoto) amesema wengi watakamatwaPicha: Imago/Xinhua Afrika

"Almuradi uchunguzi huo unaendelea kuna baadhi ya hatua ambazo zitasalia," alisema Matiang'i, "kwa mfano vituo hivyo vya televisheheni vitaendelea kuzimwa hadi uchunguzi huo ukamilike,” aliongeza waziri huyo.

Kadhalika serikali ya Kenya inasema kuondolewa kwa jeshi la polisi hapo jana katika uwanja wa Uhuru park ulikuwa mkakati wa makusudi  kuepusha umwagikaji wa damu baada ya kupata taarifa za kijasusi kuwa kulikuwa na wahalifu waliojikita chini ya mwavuli wa Muungano wa NASA.

"Hizo zilikuwa juhudi zilizopangwa vizuri zilizolenga kuzusha makabiliano na jeshi la polisi ili kusababisha umwagikaji wa damu ya wananchi wasio na hatia,” alisema Waziri huyo wa usalama wa ndani.

NRM imepigwa marufuku sasa

Wakati huo huo, serikali imepiga marufuku vugu vugu la mageuzi la Muungano wa NASA linalojulikana kama NRM. Vugu vugu hilo limetajwa kuwa linawachochea Wakenya kusababisha uhalifu kinyume cha sheria na kwamba yeyote atakayejihusisha nalo atakabiliwa na mkono wa sheria.

Demonstration in Nairobi Kenia 07.07.2014
Polisi wameanza kamata kamataPicha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo ni pigo kwa upinzani kwani chombo hicho kilichoanzishwa mwaka uliopita kilikuwa na jukumu la kuipinga serikali iliyopo madarakani na inayopingwa na muungano wa NASA. Hata hivyo wachambuzi wa masuala ya siasa wanakosoa hatua hiyo.

"Hiyo ni siasa si uongozi wajua kama hujamkamata mtu na ushahidi wa kuonesha kuwa anapanga kitu kibaya na anafanya nini huwezi kumpa jina kama hilo,” alisema Joan Sasaka mchambuzi wa masuala ya kisiasa kutoka Kenya.

Kutokana na kamatakamata iliyotangazwa, swali lililopo ni ikiwa  kiongozi wa Muungano wa NASA Raila Odinga naye atakuwa miongoni mwa waliopangiwa kukamatwa?

Mwandishi: Shisia Wasilwa

Mhariri: Yusuf Saumu