Kamanda wa Maimai awahimiza watu kujikinga dhidi ya Ebola
9 Septemba 2019Kwa mara ya kwanza kabisa, tangu kuripuka kwa homa ya Ebola katika mikoa ya Kivu ya kaskazini pamoja na Ituri kasakzini mashariki ya Congo, kamanda mmoja wa wapiganaji wa Maimai, amesimama kidete na kuwahamasisha wakaazi kujikinga dhidi ya Ebola na kutowashambulia watabibu wanaoshiriki katika vita dhidi ya homa hiyo ambayo kwa sasa imesababisha vifo vya watu zaidi ya 2000 tangu kuripuka kwa homa hiyo agosti Mwaka wa 2018.
Akiwahutubia wakaazi wa Mataba, kitongoji kilicho umbali wa kilomita 15 kusini mwa mji wa Beni, kabla ya kupata chanjo dhidi ya homa ya Ebola, jenerali Kambale Mayani wa kundi la UPLC alisema, kuwa makundi ya Maimai yanayowashambulia watabibu pamoja na kuvishambulia vituo vya afya, na yale yanayowaambia wakaazi kwamba homa ya Ebola haipo katika eneo hili, ni wauwaji sambamba na waasi kutoka Uganda ADF, wanaowauwa watu kwa kuwakata kwa mapanga katika mji na wilaya ya Beni.
Akiwaambia wakaazi wa Mataba, moja wapo ya vitongoji vinavyounganisha wilaya ya Kalunguta, kwamba yeye pamoja na wapiganaji wake wanayo kinga ya risasi, lakini kinga dhidi ya Ebola hawana na ndio maana ameamua kupata chanjo ya kukinga Ebola, aliwatahadharisha wapiganaji wake ambao wana dhana potofu kwamba Ebola haipo katika eneo hili, akiahidi kupambana nao kwa matamshi haya
Wilaya ya Kalunguta, katika wilaya ya Beni, imeshuhudia wagonjwa wa Ebola zaidi ya 180, na asili mia hamsini ya walioambukizwa wakiwa ni wakaazi wa kitongoji cha Mataba, mkuu wa wilaya hiyo Daktari Justin Muyisa Kisenge aliwaomba wakaazi wa Mataba kuwaunga mkono watabibu, ili wote kwa pamoja, yaani wakaazi pamoja na watabibu, waitokomeze homa ya Ebola katika wilaya yao ya afya
Kamanda wa Maimai UPLC, aliye na makao yake makuu Kalunguta, amechukua uamzi wa kuziunga mkono timu za watabibu katika vita dhidi ya Ebola, wakati makamanda wengine wa makundi ya hilo pamoja na wapiganaji wao, bado wanawatishia maisha watabibu katika wilaya ya Lubero.
Hapo majuzi, kijiji cha Muhangi, kilomita 40 kusini mwa mji wa kibiashara wa Butembo kilishambuliwa na Maimai, waliowatishia maisha watabibu, na kunayo taarifa kwamba, pikipiki moja inayotumiwa na watabibu katika mpango wa kukabiliana na Ebola huenda iliporwa na wanachama wa kundi hilo.
Kuwajibika kwa kamanda Kambale Mayani wa kundi la Maimai UPLC, kunadhaniwa na wengi kuwa ni hatua kubwa na muhimu inayopigwa, katika kukabiliana na Ebola katika eneo hili, makundi ya Maimai, yakiwa yanashukiwa kila mara, katika mashambulizi dhidi ya vituo vya afya wanakotibiwa wagonjwa wa Ebola, jambo linalosababisha homa hiyo kutotokomezwa haraka katika mikoa ya Kivu ya kaskazini pamoja na Ituri.
Tangu kuripuka kwa homa ya Ebola katike eneo hili agosti Mwaka jana, homa hiyo imeshagharimu maisha ya watu zaidi ya elfi mbili.