Kamanda wa jeshi la Saudia atimuliwa kwa madai ya rushwa
1 Septemba 2020Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali, SPA, Mfalme Salman wa Saudi Aabia ametoa amri ya kifalme leo Jumanne kumuondoa luteni jenerali Fahad bin Turki bin Abdulaziz, kamanda wa vikosi vya muungano katika vita nchini Yemen vinavyoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya wanamgambo wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran. Likinukulu amri hiyo ya kifalme shirika hilo limesema jenerali huyo amestaafishwa na amewekwa chini ya uchungzuzi.
Mtoto wake wa kiume, Mwanamfalme Abdulaziz bin Fahad bin Turki bin Abdulaziz Al Saud, ambaye ni naibu gavana wa jimbo la Al-Jouf, kaskazini mwa Saudia, pia ametimuliwa na kuwekwa chini ya uchunguzi.
Nafasi ya kamanda Fahad imechukuliwa na Multaq bin Salim, naibu mnadhimu wa jeshi, kutokana na mapendekezo ya mrithi mwanamfalme Mohammed bin Salman.
Kwa mujibu wa amri hiyo ya kifalme, uamuzi huo umetokana na pendekezo la mrithi mwanamfalme Mohammed bin Salman kufanya uchunguzi kuhusiana na shughuli za kifedha zilizotiliwa mashaka ambazo zilifuatiliwa katika wizara ya ulinzi. Amri hiyo ya kifalme imeongeza kusema kwamba wakala wa kupambana na rushwa Nazaha ulifichua rushwa ya fedha katika wizara hiyo inayomhusisha baba na mtoto wake wa kiume, na maafisa wengine wanne wa jeshi pia wanachungzwa kutokana na sakata hilo.
Haijabainika wazi ikiwa waliotajwa katika amri hiyo ya kifalme wameshakamatwa na wanazuiliwa. Wakala wa kupambana an rushwa Nazaha utakamilisha utaratibu wote wa kuwachunguza maafisa wote wa jeshi na wa umma wanaohusika na wanaoweza kusaidia kutoa taarifa muhimu kufanikisha mchakato huo.
Ujumbe wa wazi dhidi ya rushwa
Ali Shihabi, mwandishi wa vitabu na mchambuzi wa Saudi Arabia, amesema tangazo la kumfuta kazi kamanda huyo ni ishara ya wazi dhidi ya rushwa katika jeshi.
Tangazo hilo ni hatua ya hivi karibuni ya mapambano ya serikali ya kile ambacho maafisa wanakieleza kuwa ni rushwa iliyokithiri katika ufalme huo. Maafisa kadhaa wa usalama waliokuwa na vyeo vya juu walikuwa miongoni mwa maafisa waliofutwa kazi mwezi uliopita kwa madai ya rushwa katika miradi ya utalii.
Mwezi Machi mwaka huu, shirika la kutetea haki za binadamu Human Rights Watch lilielezea wasiwasi wake kuhusu ukamataji wa maafisa 298 wa Saudi Arabia kwa madai ya kuhusika na vitendo vya rushwa, likionya juu ya uwezekano wa kuendeshwa kesi zisizokuwa na haki katika taifa ambalo mfumo wake wa kimahakama hauko wazi.
Kwa mujibu wa wakala wa kupambana na rushwa wa Saudi Arabia, maafisa wa jeshi na idara ya mahakama walikuwa miongoni mwa waliotiwa mbaroni kwa madai ya kutoa au kupokea hongo na matumizi mabaya ya fedha za umma zinazofikia thamani ya jumla ya riyale milioni 379, ambazo ni sawa na dola milioni 101.
(dpa, afpe)