Kamanda wa Iran asema nchi hiyo haitaki vita na Marekani
2 Januari 2020Rais wa Marekani Donald Trump aliishutumu Iran kwa kuchochea maandamano katika ubalozi wa Marekani nchini Iraq siku ya Jumanne na kusema Tehran inawajibishwa. Iran imekana shutuma hizo. "Hatuielekezi nchi hii katika vita, lakini hatuogopi vita vyovyote na tunawaambia Wamarekani kwamba wazungumze vizuri na taifa la Iran.
Tuna uwezo kuwavunja mara kadhaa na hatuna hofu," kamanda wa jeshi la mapinduzi ya Iran brigadia jenerali Hossein Salami alinukuliwa na shirika hilo la habari la Tasnim akisema. Trump alisema katika ukurasa wa Twitter siku ya Jumanne kuwa Iran "itawjibishwa kikamilifu kutokana na vifo, ama uharibifu utakaotokea, katika majengo yetu yoyote. Watalipa kwa gharama kubwa ! Hii si tahadhari, hiki ni kitisho." Baadaye alisema hataki vita ama kutarajia kuingia vitani na Iran.
Kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ayatollah Ali Khamenei jana alishutumu mashambulizi ya Marekani dhidi ya wanamgambo washirika wa Iran nchini Iraq, akiilaumu Marekani kwa matumizi ya nguvu katika nchi hiyo jirani ya Iraq.
Iran ililalamika jana kwa mjumbe wa Uswisi , ambaye anawakilisha maslahi ya Marekani mjini Tehran, kuhusiana na kile ilichokiita, "matamshi ya kuchochea vita" yanayotolewa na maafisa wa Marekani.
Uwiano tete
Iraq imekuwa ikipata taabu kujiweka katika uwiano tete kati ya washirika wake Iran na Marekani wakati hali ya wasi wasi ikiongezeka kufuatia kujiondoa kwa Marekani katika makubaliano ya kinyuklia ya mwaka 2015 na Iran.Uhasama wa kikanda kwa sehemu fulani unaonekana katika majeshi ya usalama ya Iraq; Marekani imetoa mafunzo kwa jeshi la nchi hiyo, wakati Iran imekuwa ikitoa msaada jeshi la Kundi la Hashed al-Shaabi.
Jeshi hilo limeasisiwa mwaka 2014, na jeshi la hashed rasmi ni sehemu ya majeshi ya serikali ya Iraq na kiongozi wake mkuu Faleh al-Fayyadh , pia anatumika kama mshauri wa taifa wa usalama.
Maafisa wa Marekani na Iraq wameliambia shirika la habari la AFP kwamba wanashangaa kuona vikosi vya jeshi la Hashed kuwekwa katika wiki za hivi karibuni ndani ya eneo la kanda ya kijani, Green Zone, eneo linalolindwa ambalo lina ofisi za serikali na balozi za nje, na pia ofisi za Umoja wa Mataifa.
Kuingiliwa kwa viunga vya ubalozi wa Marekani mjini Baghdad kumesababisha waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike pompeo kuahirisha ziara yake nchini Ukraine pamoja na mataifa mengine manne. Pompeo alitarajiwa kuwasili nchini Ukraine leo Alhamis.