KALFOU,Niger: Jumuiya ya kimataifa yalaumiwa kwa maafa ya njaa
31 Julai 2005Ufaransa imelaumu maafa ya ukosefu wa chakula yalioikumba koloni lake la zamani Niger kuwa yametokana na kuchelewa kwa jumuiya nzima ya kimataifa kuitikia kilio cha nchi hiyo na kusema kwamba Ufaransa sio nchi pekee inayowajibika kuzisaidia nchi za kimaskini duniani.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Philippe Douste-Blazy amesema nchi yake itaongeza maradufu msaada wa chakula kwa nchi hiyo hadi kufikia euro milioni 4.6 sawa na dola milioni 5.6 za Marekani. Waziri huyo amesema Rais Jacques Chirac wa Ufaransa alikuwa ni mkuu pekee wa nchi kulifikisha suala la Niger katika mkutano wa Viongozi wa Kundi la Mataifa Manane tajiri duniani huko Scotland mwezi huu.
Njaa katika nchi hiyo iliokumbwa na ukame na kuvamiwa na nzige inatishia maisha ya maelfu ya watoto na imewaacha mamilioni ya watu bila ya kuwa na chakula.
Wataalamu wanasema asilimia 30 ya idadi ya watu wa Niger wanakabiliwa na njaa.