Kaka wa Brazil ndie stadi 2007
18 Desemba 2007Mechi za mwisho za kuania nafasi ya duru ijayo ya kombe la UEFA-kombe la shirikisho la dimba la Ulaya, zitachezwa kesho jumatano huku viongozi wa Ligi wa Ujerumani-Bayern Munich,wakiikaribisha nyumbani Allianz Arena,Aris Saloniki ya Ugiriki na ikihitaji sare tu kusonga mbele.
Kaka, stadi wa Brazil kama ilivyotarajiwa alitawazwa jana usiku mjini zurich,Uswisi „mchezaji bora wa mwaka wa dunia“ akiwapiku akina Christiano Ronaldo wa Ureno na Lionel Messi wa Argentina.
Uganda inaumana leo na Kenya katika robo-finali ya kombe la challenge Cup baada ya jana Sudan,mabingwa kuwatimua Taifa Stars,Tanzania.
Kundi F la UEFA ndilo gumu kuliko yote huku klabu 3 kati ya 4 zikinyan’ganyia nafasi 3 zilizobaki na ni Red Star Belgrade tu ambayo haina nafasi.
Mabingwa kadhaa wa Ujerumani Bayern Munich watatamba kesho nyumbani wakiwakaribisha wagiriki Aris Saloniki kwa sherehe ya mwisho ya dimba kabla ya X-masi.Munich inahitaji kutoka sare tu na pointi 1 kukata tiketi ya duru ijayo ya UEFA cup.
Nafasi 3 zinazoaniwa katika kundi F zimeshanyakuliwa na Spartak Moscow,Zurich na klabu nyengine ya Ujerumani Bayer Leverkusen.
Kesho Hamburg itaumana na Basle ya uswisi kuamua nani ataparamia killeni mwa ngazi ya kundi la D.Hamburg imeshinda mechi zake zote 3 hadi sasa katika kundi hili na kama bayern munich kesho, wanahitaji Hamburg sare na pointi 1 kukata tiketi yao ya duru ijayo.
Stadi wa Brazil na mchezaji wake wa kiungo-Kaka ndie „mwanasoka bora wa mwaka wa dunia“ na jana alikamilisha kuzoa mataji yote ya dimba kwa mwaka huu.Kwani, taji la mchezaji bora wa FIFA lilifuatia lile la golden ball la Ulaya.Kaka alimshinda Muargentina Lionel Messi na mreno Cristiano Ronaldo wa Manchester United.Mastadi hao 3 waliteuliwa katika finali kutoka kundi la mastadi 30 na hilo likawa taji lake la 3 mwaka huu kwa kaka.Taji lake la 3 ni lile la jarida la dimba la dunia world soccer magazin. Rais wa FIFA –shirikisho la dimba ulimwenguni Sepp Blatter akimtangaza mshindi mjini Zurich alisema:
„Mabibi na mabwana-mshindi ni…Kaka“.
Akitoa shukurani zake kwa ndoto asioitazamia:Kaka alisema:
„Huu ni usiku maalumu kwangu.sabbu nilipokua chipukizi,ndoto yangu ilikua kuwa mchezaji-dimba wa kulipwa kwa klabu ya Sao Paulo na kuichezea alao mara moja timu ya Taifa ya Brazil na si zaidi.
Lakini, Biblia yasema:neema za Mwenyezi mungu hazihesabiki na hii ndio neema yake maishani mwangu.“
Alielezea Kaka wa Brazil,stadi wa Ac Milan alieitawaza majuzi kuwa mabingwa wa klabu bingwa ya dunia huko Yokohama kwa mabao yake maridadi ajabu.
Robo-finali ya challenge cup-kombe la klabu bingwa barani Ulaya iliendelea leo mjini Dar-es-salaam,Tanzania kwa majirani wawili Uganda kumenyana na Harambee Stars-Kenya.Kenya iliingia robo-finali chupuchupu tu kwa kuitoa Somalia kwa mabao 2:0.Uganda ikitamba tangu awali na ndio iliotia mabao mengi kabla ya changamoto ya leo.
Zanzibar Heroes –timu iliozusha maajabu hadi sasa kwa kwenda sare na mabingwa watetezi Sudan na kuipiga kumbo Ethiopia,walikuwa na miadi leo na Ruanda ambao waliwapelekea salamu wazanzibari visiwani tena na mapema kwamba wao si Ethiopia wala Sudan.
Sudan lakini ndio waliowan’goa jana meno kaka zao -Tanzania bara walipowachezesha kindumbwendumbwe na kuwatimua nje kwa mabao 2:1 huko huko mzizima.
Hatima ya timu ya pili ya Tanzania-Zanzibar katika kinyan’ganyiro hiki inajulikana leo sawa na ile ya Harambee Stars.
Kombe la Afrika la Mataifa likikurubia mwezi ujao, rais John Kufour wa Ghana aliufungua mwishoni mwa wiki rasmi uwanja mpya mjini Kumasi wa Baba Yara.Ukichukua hadi mashabiki wa mpira 40,000 uwanja huo utachezewa mapambano ya kundi C na baadae robo-finali na hata nusu-finali na ule wa kuamua nafasi ya tatu.Uwanja wa Baba yara ulifunguliwa kwa dimba kati ya Blacks Stars na Tembo wa Ivory Coast walioikanyaga nyota jeusi na kuitia dosari kwa mabao 2:0 kabla firimbi kulia rasmi Januari 20.
FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni,limechapisha orodha yake ya mwezi ya timu bora:Nigeria iko kileleni ikifuatwa na simba wa nyika-Kamerun.Guinea yafuata nafasi ya 3 huku Ivory Coast ikibidi kuridhika na nafasi ya 4.Katika kanda ya Afrika mashariki,Uganda iko nafasi ya 16,Tanzania 21,Burundi ya 30 wakati Kenya 31.Comoro iko nafasi ya 51 ikiachia Somalia kuburura mkia katika nafasi ya 52.