Kagame kuiongoza Rwanda hadi 2034?
30 Oktoba 2015Hii kutangazwa kwa uamuzi huu umehitimisha safari ya miezi mitatu iliyoanza mwezi wa saba ambapo bunge la Rwanda lilianza mchakato mchakato wa mabadiliko ya katiba. Akizungumza bungeni baada ya kupitisha uamuzi huo, spika wa bunge la Rwanda Donatille Mukabarisa amesema: "Tumeweka muhula wa miaka saba pekee ambayo unafuata muhula huu unaomalizika na unaozungumziwa kwenye kipengele kilichotangulia. Tumeuweka muhula huu kama wa mpito tu kwa sababu kwa mujibu wa sheria kunapotokea mabadiliko ni lazima kuwepo na kipindi cha kuweka mambo sawa, na hii ni kwa sababu tunataka kuelekea kule tunakopenda."
Katiba ya Rwanda kulingana na nchi za Afrika Mashariki
Uamuzi huo umeridhiwa na wabunge wote 80 wa wabunge la Rwanda lakini mjadala uliochukua muda ni ule kuhusu baadhi ya vipengele vingine hasa kile kinachohusu hatima ya Rais anapostaafu. "Ni lazima tutazame pia mahitaji zaidi kwa rais anayeomba kuwa seneta baada ya kumaliza muhula wake kwa sababu kuwahi kuwa Rais hakupaswi kumpa mtu tiketi ya moja kwa moja ya Rais na hii ni kwa sababu anaweza kuwa alifanya mambo ambayo hayawezi kumruhusu kufanya kazi hiyo ya useneta," amesema mbunge mmoja.
Mabadiliko haya ya katiba yanakwenda mbali na kusema kwamba baada ya muhula huo wa miaka saba Rwanda itaendelea na mihula ya miaka mitano inayompa Rais nafasi kugombea mara mbili tu. Lakini la miaka saba na miaka mitano likaonekana kwuachanganya baadhi ya wananchi.
Spika wa bunge amesema kimsingi wabunge wamepitisha uamuzi huo ili kwamba baadaye katiba ya Rwanda iende sambamba na nchi nyingine za Jumuiya ya Afrika Mashariki hasa kuhusu mihula ya miaka 5 ya urais. Kutokana na mabadiliko haya huenda sasa Rais Paul Kagame akaitawala Rwanda hadi mwaka 2034.