Kabul.Wapiganaji wauwawa na majeshi ya NATO.
29 Oktoba 2006Majeshi ya Afghanistan na yale ya NATO yamewauwa zaidi ya wapiganaji 55 katika mapigano ambayo yamehusisha helikopta pamoja na ndege za kijeshi, wakati ambapo mwanajeshi mmoja wa mataifa ya nje ameuwawa na wengine wanane wamejeruhiwa katika shambulio la bomu.
Maafisa wa kijeshi nchini Afghanistan wamesema kuwa matukio hayo tofauti yametokea jana Jumamosi katika jimbo la kaskazini la Uruzgan, ambako jeshi la kimataifa la kusaidia kuimarisha usalama limeweka wanajeshi wa Australia na Uholanzi.
Wakati huo huo , Jenerali wa jeshi la NATO James Jones ameomba radhi kutokana na vifo vya raia katika shambulio lililolenga wapiganaji wa Kitaliban katika jimbo la Kandahar siku ya Jumanne.
Lakini Jones pia amewalaumu wapiganaji kwa kuwatumia raia wa kawaida kama ngao yao.
Rais wa Afghanistan Hamid Karzai ameiteua tume ya kuchunguza tukio hilo la Kandahar, ambalo wizara ya mambo ya ndani imesema limeuwa raia zaidi ya 20.