KABUL:Raia 19 wa Korea kusini wakutana pamoja baada ya kuachiwa
31 Agosti 2007Raia 19 wa Korea Kusini walioshikwa mateka na kundi la Taleban wamekutana pamoja katika eneo la siri baada ya kuzuiliwa kwa wiki sita.Korea Kusini inalaumiwa kwa kufanya majadiliano na wapiganaji hao wa Taleban ili raia wake waachiwe.
Wafanyikazi hao wa misaada waliachiwa kwa awamu kuanzia siku ya Jumatano na hapo jana katika maeneo tofauti mkoani Ghazni.Ni wakati huo waliweza kufahamu kuwa wanaume wawili waliokamatwa nao Julai 19 walipigwa risasi hadi kufa.
Wanaume hao wawili kasisi mmoja wa umri wa miaka 42 na mmisheni aliye na umri wa miaka 29 walipigwa risasi katika kipindi cha majuma mawili.Kundi la Taleban lilichukua hatua hiyo ili kuishinikiza serikali kuwaachia wafungwa wao jambo lililopingwa vikali na halijatimizwa.
Kulingana na walinzi katika hoteli ya kifahari ya pekee mjini Kabul kundi la kwanza la raia hao wa Korea Kusini limeshawasili na wako chini ya ulinzi mkali japo taarifa hizo hazijathibitishwa.
Kuachiwa kwa mateka hao kunatokea baada ya mazungumzo kati ya wawakilishi wa kundi la Taleban na ujumbe wa Korea Kusini yaliyofanyika mjini Ghazni.Serikali ya Korea Kusini kwa upande wake imeahidi kuondoa majeshi yake 200 wanaohudumu katika vitengo vya uhandisi na utabibu ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.
Kulingana na gazeti moja la Japan Korea Kusini iliwapa kundi la Taleban dola milioni 2 baada ya wasuluhishi kusema kuwa malipo ndio njia ya pekee ya kuwanusuru mateka hao.Viongozi wa Taleban vilevile serikali ya Afghanistan wanakanusha madai hayo.
Ujerumani kwa upande wake inashtumu namna Korea Kusini ilivyosuluhisha tatozo hilo huku Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akishikilia kuwa nchi yake haitajadiliana na Taleban ili mhandisi wake aachiwe.Mhandisi huyo alikamatwa zaidi ya majuma 6 yaliyopita.