KABUL:Miili ya wanajeshi 17 wa Uhispania yarejeshwa nyumbani.
18 Agosti 2005Miili ya wanajeshi 17 wa Uhispania waliouawa baada ya helikopta yao kuanguka magharibi mwa Afghanistan,imesafirishwa leo kupelekwa nyumbani.
Waziri wa Ulinzi wa Uhispania,Jose Bono,ambaye alikwenda Afghanistan mara tu ilipotokea ajali hiyo siku ya Jumanne,pia yumo katika ndege hiyo,inayorudisha nyumbani mabaki ya wanajeshi wa nchi yake.
Serikali ya Uhispania awali ilikuwa ikihisi kuwa helikopta hiyo ilianguka baada ya kushambuliwa na wanmgambo.Lakini Bwana Bono,amesema uchunguzi uliofanywa umeweza kugundua hakukuwepo na ushahidi wa kuhusisha kuanguka kwa helikopta hiyo na kushambuliwa.Amesema huenda helikopta hiyo ulianguka kutokana na upepo mkali uliokuwa ukivuma.
Wanajeshi hao waliokufa katika ajali hiyo walikuwa ni sehemu ya wanajeshi wa Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi-NATO yaliyopo nchini Afghanistan.