KABUL.KIongozi wa Taliban avionya vikosi vya NATO viondoke Afghanistan
23 Oktoba 2006Kiongozi wa kundi la Taliban Mullah Mohammed Omar ameamrisha kuwa wanajeshi wa muungano wa NATO waondoke kutoka nchini Afghanistani la sivyo ameonya kuwa majeshi hayo yatakabiliwa na mashambulio makali baada ya kumalizika kwa mwezi mtukufu wa ramadhan.
Ujumbe huo uliotolewa kupitia shirika moja la habari la nchini Pakistan uliongeza kusema kuwa rais wa Afghanistan Hamid Karzai atashtakiwa mbele ya mahakama ya kiislamu.
Mullah Omar yuko mafichoni tangu mwaka 2001.
Wakati huo huo wanajeshi wa muungano wa NATO wamewauwa waasi 15 katika jimbo la Zabul kusini mwa Afghanistan.
Habari zaidi kutoka Afghanistan zinasema ubalozi wa Italia umesema kuwa muda wa siku kumi uliowekwa na watu waliomteka nyara mwandishi wa kitaliani Gabriele Torsello huko kusini mwa Afghanistan umepita.
Watekaji nyara hao wanaitka Italia kuyaondoa majeshi yake kutoka nchini humo.
Umoja wa mataifa umesema takriban dola milioni 43 zinahitajika kununulia chakula kwa zaidi ya watu milioni 1.9 wa Afghanistan kabla ya msimu wa baridi kali kuanza.