1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kabul: Wanamgambo wa Taliban watarajiwa kukutana na maafisa wa Korea Kusini kuhusu mateka.

2 Agosti 2007
https://p.dw.com/p/CBct

Wakuu wa Korea Kusini na Afghanistan wanashauriana kuhusu mahali pa kukutana baada ya kukubaliana kukutana ana kwa ana na wanamgambo wa Taliban wanaowashikilia mateka ishirini na mmoja raia wa Korea Kusini.

Mkuu wa ujumbe wa Taliban kwenye mashauriano hayo, Waheedullah Mujadidi, amesema kundi lake limekubali kukutana na balozi wa Korea Kusini.

Tarehe nyingine ya mwisho iliyotolewa na wanamgambo wa Taliban ilikuwa jana, lakini hakuna mateka mwingine aliyeuawa.

Mateka wawili wameshauawa baada ya kupita tarehe iliyowekwa na Taliban ya kuwaachia huru wanamgambo walio magerezani.

Wakati huo huo, maiti ya mateka wa pili raia wa Korea Kusini aliyeuawa na wanamgambo wa Taliban nchini Afghanistan, inatarajiwa kuwasili nchini Korea Kusini leo.

Wabunge wa Korea Kusini wameelekea nchini Marekani kuiomba serikali hiyo iingilie kati suala la mateka wa Korea Kusini wanaoshikiliwa na wanamgambo wa Taliban, tangu majuma mawili yaliyopita.