1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

KABUL : Waislamu waandamana kupinga kufuru kwa Quran

14 Mei 2005
https://p.dw.com/p/CFDt

Kumekuwepo na maandamano ya hasira katika ulimwengu wa Kiislam kuanzia Indonesia hadi Gaza hapo jana kutaka kulipizwa kisasi kufuatia repoti kwamba wasaili wa Marekani katika Ghuba ya Guantanamo wameikufuru Quran.

Nchini Afghanistan watu tisa wameuwawa hapo jana katika maandamano kufuatia repoti hiyo na kufanya idadi ya vifo kufikia watu 16 wiki hii katika maandamano mabaya kabisa kuwahi kufanywa dhidi ya Marekani tokea kuanguka kwa utawala wa Taliban.

Serikali ya Marekani imekuwa mbioni kutaka kudhibiti hasira hiyo ya Waislamu wakati washirika wake wakitaka ifanye uchunguzi huku maelfu wakiingia mitaani kutokana na kughadhibishwa na repoti ya gazeti la Newsweek kwamba wasaili katika gereza la Marekani huko Ghuba ya Guantanamo wamekiweka kitabu hicho kitukufu cha Waislamu chooni pamoja na kukitumbukiza kwenye lindi.

Maandamano hayo yamezagaa hadi Pakistan ambayo imeitaka Marekani ichunguze suala hilo mamia ya watu pia wamefanya maandamano ya amani nchini Indonesia taifa lenye idadi kubwa kabisa ya Waislamu duniani.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Scott McCellan amesema serikali ya Marekani inayachukulia madai hayo kwa uzito mkubwa na ameyakinisha kwamba wizara ya ulinzi imeanzisha uchunguzi huku Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Condoleeza Rice akisema kwamba kutoheshimiwa kwa Quran Tukufu ni jambo ambalo Marekani haitolivumilia katu.