KABUL: Waafghanistan wanane wauwawa katika shambulio la majeshi ya NATO
18 Oktoba 2006Matangazo
Shambulio la angani la jeshi la NATO limewaua raia takriban wanane wa Afghanistan katika mkoa wa Kandahar kusini mwa nchi hiyo. Raia wengine tisa wamejeruhiwa katika hujuma hiyo.
Gavana wa mkoa wa Kandahar, Asadullah Khalid, amesema vifo hivyo vimesababishwa na mabomu ya NATO yaliyoyapiga makaazi matatu katika wilaya ya Zhari mkoani humo.
Shirika la NATO limesema linajutia vifo vya raia hao na linafanya kila juhudi kupunguza uwezekano wa kutokea maafa wakati wa operesheni zake.