KABUL : NATO kutuma zaidi ya wanajeshi 10,000 Afghanistan
6 Oktoba 2005Umoja wa Kujihami wa Mataifa ya Magharibi NATO utapeleka zaidi ya wanajeshi 10,000 nchini Afghanistan.
Katibu Mkuu wa mataifa wanachama 26 wa NATO Jaap de Hoop Scheffer amewaambia waandishi wa habari leo hii kwamba kutanuliwa kwa Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa Ulinzi ISAF kinachoongozwa na NATO katika eneo tete la kusini mwa Afghanistan kutapelekea kuwasili kwa vikosi ziada elfu kadhaa vya NATO.
Baada ya mazungumzo yake na Rais Hamid Karzai Katibu Mkuu huyo wa NATO hakutowa idadi halisi ya vikosi hivyo ila amesema vitapindukia 10,000 au kati ya 13,000 na 14,000 hadi 15,000.
Kikosi cha ISAF kimekuwepo nchini Afghanistan tokea mwaka 2001 muda mfupi baada ya kupinduliwa kwa utawala wa Taliban na kimekuja kuwa chini ya udhibiti wa NATO hapo mwaka 2003.
Idadi ya wanajeshi wake hivi sasa inafikia 10,000.