KABUL: Majeshi ya NATO yaanza operesheni dhidi ya Taliban
6 Machi 2007Majeshi yanayoongozwa na shirika la NATO nchini Afghanistan yameanza operesheni dhidi ya wanamgambo wa Taliban katika mkoa wa kusini wa Helmand nchini humo.
Operesheni hiyo inayowajumulisha wanajeshi 5,500 wa jeshi la NATO na wanajeshi wa Afghanistan, imeanza saa kumi na moja alfari ya leo. Harakati hiyo inayofanywa kufuatia ombi la serikali ya Afghanistan, imeelezwa kuwa kubwa zaidi kuwahi kufanywa nchini humo na itawalenga wapiganaji wa Taliban na biashara ya bangi.
Operesheni hiyo iliyopewa jina la Achilles ni ya kuboresha usalama mkoani Helmand, ambako wanamgambo wa Taliban waliyateka maeneo kadhaa mwanzoni mwa mwezi uliopita.
Wakati haya yakiarifiwa, raia tisa wameuwawa kwenye shambulizi la bomu katika mkoa wa Kapisa kaskazini mwa mji mkuu Kabul.
Naibu wa gavana wa mkoa huo, Sayed Mohammad Hashimi, amesema shambulio lililofanywa na jeshi la Marekani limeyalenga makaazi ya wanamgambo wa Taliban wanaofanya mashambulizi ya maroketi dhidi ya kambi za majeshi ya muungano zilizo karibu.