Kabul. Karzai awapandishia wanajeshi wa NATO.
24 Juni 2007Rais wa Afghanistan Hamid Karzai ameyakosoa sana majeshi ya NATO kuhusiana na mauaji dhidi ya raia yaliyosababishwa na kile alichokiita kushindwa kushirikiana.
Akisema kuwa maisha ya Wafghani si kitu cha kuuzwa rahisi, Karzai amewaambia waandishi wa habari kuwa majeshi ya NATO hayakuwa yakifanya uratibu na serikali ya Afghanistan katika operesheni zake.
Amesisitiza kuwa jeshi la NATO linapaswa kuliimarisha zaidi jeshi la Afghanistan na kujenga jeshi imara la polisi, ambalo litapatikana kutoka katika jamii ya nchi hiyo. Bwana kazrai amelaumu mtindo wa uhamishaji wa viwango vya mataifa ya magharibi na kuvitumia katika nchi ya Afghanistan . Amesema kuwa Afghanistan ni nchi tofauti yenye jamii na utamaduni tofauti. Amesisitiza kuwa watendaji wa jeshi la NATO wanapaswa kuanzia sasa kusikiliza kile Afghanistan inachotaka kifanyike.
Ukosoaji huo unakuja baada ya zaidi ya raia 90 wa Afghanistan kuwawa kutokana na hatua za kijeshi za majeshi hayo ya kigeni katika muda wa wiki moja.
Katika jimbo la mashariki la Paktia, zaidi ya wapiganaji wa Taliban 60 wameuwawa katika mashambulizi ya anga ya jeshi la NATO pamoja na lile la ardhini.Nayo Pakistan inasema kuwa kiasi cha watu kumi wameuwawa kwa risasi kutoka katika mpaka wa Afghanistan.
Kusini mwa Afghanistan , wanajeshi wawili wa Estonia wameuwawa na wengine wanne wamejeruhiwa katika shambulio la kombora.