1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Junta waahidi kuandaa uchaguzi Niger.

Halima Nyanza22 Februari 2010

Utawala mpya wa Kijeshi nchini Niger umeahidi kuandaa uchaguzi na katiba mpya pamoja na kurejesha demokrasia nchini humo, lakini hata hivyo haukutaja tarehe ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

https://p.dw.com/p/M7f5
Magari ya kijeshi yakionekana katika mitaa ya mji mkuu wa Niamey, nchini Niger, baada ya wanajeshi kuchukua madaraka, katika mapinduzi yaliyotokea wiki iliyopita.Picha: AP

Akizungumza baada ya kukutana na Utawala huo mpya wa Kijeshi, Rais wa Jumuia ya Kichumi ya Nchi za Afrika magharibi -ECOWAS- Mohamed ibn Chambas amesema uongozi umeahidi pia kuvishirikisha vyama vya siasa na Jumuia za raia, katika mazungumzo ya kuiandaa katiba mpya ya nchi hiyo.

Amesema wamejadiliana na viongozi hao, jinsi nchi hiyo itakavyorudi katika mfumo wa kawaida wa kufuata katiba haraka iwezekanavyo, na utawala huo umewahakikishia kutimiza hayo na kwamba hayo yote yatafanyika kwa kushirikisha jumuia hizo za kiraia na vyama vya kisiasa.

Mkutano huo na Viongozi hao wa kijeshi pia uliwashirikisha mwakilishi wa Umoja wa Mataifa Said Djinnit na Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia usalama na amani Ramtane Lamamra.

Kufuatia mazungumzo hayo, mmoja wa viongozi hao wa utawala wa kijeshi Kanali Djibrilla Hamidou Hima aliwaambia waandishi wa habari kuwa Rais aliyepinduliwa Mamadou Tandja ambaye bado anashikiliwa katika makaazi ya Rais mjini Niamey, hali yake inaendelea vizuri na kwamba Shirika la Msalaba mwekundu limeruhusiwa kumuona.

Aidha, amesema aliyekuwa Waziri Mkuu wa na mawaziri wa Mambo ya ndani na wa fedha ambao walikamatwa pamoja na Rais Tandja wakati wa mkutano wa Baraza la Mawaziri siku ya Alhamisi, bado wanachunguzwa kwa ajili ya usalama wao.

Chama cha Rais Tandja kimetaka kuachiliwa haraka kwa kiongozi huyo na bila ya masharti yoyote.

Mapinduzi nchini Niger, yalitokea siku ya Alhamisi, baada ya wanajeshi waliokuwa wakiipinga serikali ya nchi hiyo, kushambulia makaazi ya Rais, na kumteka Rais Mamadou Tandja mwenye umri wa miaka 71, ambaye alikuwa akijaribu kung'ang'ania kubaki madarakani baada ya kumalizika kwa awamu yake ya uongozi.

Utawala huo wa kijeshi nchini Niger, umekuwa ukiungwa mkono kwa kiasi kikubwa na raia, ambapo maelfu ya watu waliandamana jana nchini humo, kuunga mkono utawala huo mpya.

Rais Tandja aliyepinduliwa aliingia madarakani katika chaguzi zilizozingatiwa kuwa huru na za haki.

Utawala huo mpya wa kijeshi nchini Niger, umesema kwamba umechukua madaraka ili kurejesha utulivu nchini humo, na kama ilivyokuwa mapinduzi ya mwaka 1999, wataharakisha kurudisha utawala wa kiraia.

Kwa sasa mji mkuu wa Niger Niamey, umeelezwa kuwa tulivu, na kwamba licha ya Jumuia ya Kimataifa kulaani mapinduzi hayo, Wa Niger wengi wanaonesha kuunga mkono wanajeshi hao.

Mwandishi: Halima Nyanza(dpa, afp)

Mhariri: Abdul-Rahman,Mohammed