1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juncker ateuliwa kuwa rais wa Umoja wa Ulaya

28 Juni 2014

Jean-Claude Juncker ameteuliwa kuwa rais mpya wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya akiungwa mkono na viongozi wa Umoja huo,na kuwa pigo kubwa kwa David Cameron ambaye amekuwa akimpinga.

https://p.dw.com/p/1CRpF
Jean-Claude Juncker in Berlin 05.04.2014
Jean-Claude Juncker ameteuliwa kushika wadhifa wa rais wa halmashauri ya EUPicha: Getty Images

Hali hiyo inatishia kuongezeka kwa nafasi ya Uingereza kujitoa kutoka kundi hilo la mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu wa Uingereza ameuita uteuzi wa Juncker kuwa ni "Kitu kibaya kwa Ulaya " na amesema huenda ukazuwia juhudi zake za kuiweka Uingereza katika Umoja wa Ulaya kabla ya kura ya maoni ya kuitoa ama kuibakisha nchi hiyo katika umoja huo , zoezi litakalofanyika mwaka 2017.

EU Gipfel David Cameron 27.06.2014
David Cameron anampinga JunckerPicha: Reuters

Juncker aungwa mkono na wote

Juncker , waziri mkuu wa zamani wa Luxembourg na mwanasiasa mwenye kujua mambo kwa undani katika Umoja wa Ulaya, ameungwa mkono na mataifa yote ya Umoja huo isipokuwa Uingereza na Hungary.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel , ambaye baadhi nchini Uingereza wanamlaumu kwa kumyumbisha Cameron kwa kubadilisha misimamo yake kuhusu Juncker , amesifu uzoefu wake, akisema atasikiliza matakwa ya mataifa wanachama na bunge la Ulaya.

Kanzlerin Angela Merkel Schweden Pressekonferenz Harpsund
Angela Merkel ana nguvu kubwa katika bara la UlayaPicha: Reuters

"Nina vutiwa mno na Uingereza kubakia mwanachama wa Umoja wa Ulaya . Katika hisia hizi nitaendelea kufanyakazi," pia amesema, akiepuka mapambano ambayo viongozi wa ulaya wanakumbana nayo hivi sasa kuukarabati uhusiano na Cameron kabla ya kura ya maoni nchini Uingereza.

Cameron bado hakubaliani

Lakini Cameron anaendelea kusimama katika msimamo wake katika upinzani wake dhidi ya uteuzi wa Juncker kuwa mkuu wa halmashauri tendaji ya Umoja wa Ulaya.

"Inatishia kuyumbisha msimamo wa serikali za kitaifa, inatishia kuyumbisha nguvu za mabunge ya taifa na inatoa nguvu mpya kwa bunge la Ulaya," Cameron amewaambia waandishi habari.

Akiulizwa iwapo Uingereza sasa iko karibu ya kujitoa kutoka Umoja wa Ulaya , amesema : Kazi imekuwa ngumu ya kuiweka Uingereza katika Umoja wa Ulaya ulioingia katika mabadiliko.... Je ninafikiri ni kazi ambayo haiwezekani? Hapana."

Magazeti ya Uingereza leo Jumamosi (28.06.2014)yote yamekubaliana na mawazo kwamba nchi hiyo inakaribia kujitoa kutoka katika Umoja wa Ulaya baada ya Cameron "kushindwa vibaya" kuzuwia uteuzi wa Juncker.

EU Parlamentswahl 25.05.2014 Juncker
Jean-Claude JunckerPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Hata gazeti ambalo kwa kiasi kikubwa linapendelea Umoja wa Ulaya la Independent limeonya kuhusu kuongezeka kwa uwezekano wa kujitoa kwa Uingereza kutoka kundi hilo la mataifa kwa kuandika , " Cameron ashindwa, na Uingereza yaelekea ukingoni mwa kutoka kutoka Umoja wa Ulaya."

Magazeti yametofautiana kuhusu iwapo Uingereza itakuwa katika hali nzuri katika hali ya "kutengwa", baadhi yakisema jinsi Cameron alivyolishughulikia suala la Juncker litafanya kuwa vigumu kwake kufanya majadiliano kuhusu masharti ya uanachama wa Umoja wa Ulaya.

Uingereza huenda ikapewa nafasi ya juu ya uongozi Brussels

Viongozi wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kujaribu kumfurahisha Cameron, hususan kwa kutoa kwa Uingereza nafasi ya juu ya cheo katika uongozi wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels katika mkutano mwingine utakaofanyika mwezi ujao ambao utaamua duru nzima ya viongozi wakuu wa Umoja wa Ulaya mjini Brussels.

Tofauti kuhusu Juncker imekuja mwezi mmoja baada ya vyama vinavyopinga Umoja wa Ulaya kupata mafanikio katika uchaguzi wa Ulaya, wakati chama cha UK Independence nchini Uingereza kikipata ushindi wa moja kwa moja na chama cha National Front nchini Uingereza .

Mini-Gipfel in Schweden Merkel im Boot Symbolbild in einem Boot sitzen
Merkel akiwa katika boti pamoja na viongozi wengine wa EUPicha: Reuters

Merkel kiongozi mwenye nguvu barani Ulaya , amewataka wenzake wa Umoja wa Ulaya "kuiridhia" Uingereza.

Na Cameron ameapa kuendelea kuhimiza mageuzi katika Ulaya kama kurejesha baadhi ya madaraka kwa nchi husika kabla ya kura ya maoni.

Cameron pia ameahidi kufanyakazi pamoja na Juncker, licha ya kumueleza kama " mtu wa ndani anayehusika zaidi na Umoja huo".

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Amina Abubakar