1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Viongozi waonyesha matumaini

23 Juni 2015

Matumaini ya Ugiriki kupatana na wakopeshaji wake wa kimataifa yamejitokeza baada ya Ugiriki kuyawasilisha mapendekezo mapya yaliyozingatiwa kwenye kikao cha dharura cha viongozi wa nchi za ukanda wa sarafu ya Euro .

https://p.dw.com/p/1FlyV
Viongozi wakutana kuijadili Ugiriki
Viongozi wakutana kuijadili UgirikiPicha: Reuters/E. Durand

Baada ya kikao chao cha dharura mjini Brussels viongozi wa nchi za ukanda wa sarafu ya Euro sasa wamewapa mawaziri wao wa fedha jukumu la kufanya mazungumzo mengine hapo kesho ili kuyafafanua masuala yote kwa kirefu, kabla ya kufanyika mkutano muhimu sana wa viongozi wa nchi zote 28 za Umoja wa Ulaya hapo Alhamisi. Mustakabali wa Ugiriki katika ukanda wa sarafu ya Euro na hatimaye katika Umoja wa Ulaya utaamuliwa kwenye mkutano huo.

Baada ya kikao cha jana mjini Brussels Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Jean-Claude Juncker amesema anao uhakika kuwa mvutano baina ya serikali ya Ugiriki ya mrengo wa kushoto na wadai wake uliochukua muda wa miezi mitano utamalizwa . Juncker amesema anao uhakika kwamba makubaliano kamili yatafikiwa mnamo wiki hii kwa sababu ameeleza kuwa ni lazima wapate suluhisho mnamo wiki hii.

Amesema anao uhakika kwamba nchi za ukanda wa sarafu ya Euro Jumatano ijayo zitafikia matokeo yatakayowasilishwa kwa Baraza la Umoja wa Ulaya Alhamisi ijayo.Juncker amesema uamuzi utafanywa mnamo wiki hii

Ugiriki yawasilisha mapendekezo mapya muhimu

Matumaini hayo yanatokana na mapendekezo mapya yaliyowasilishwa na Ugiriki kwenye mkutano wa kilele wa viongozi wa ukanda wa sarafu ya Euro. Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema mapendekezo hayo ni hatua ya kusonga mbele lakini ameeleza kuwa kazi kubwa bado inahitaji kufanyika.

Ugiriki sasa imekubali kupandisha kodi ya makampuni na kuondoa nafuu ya kodi kwa taasisi kadhaa. Aidha imesema katika mapendekezo yake kwamba umri wa kustaafu utapandishwa hatua kwa hatua hadi kufikia miaka 67. Lakini Kansela Merkel amesema suala la Ugiriki kupunguziwa madeni halipo asilani kama jinsi Ugiriki ilivyokuwa inapendekeza hapo awali.

Baada ya kuyawasilisha mapendekezo ya nchi yake Waziri Mkuu wa Ugiriki Alexis Tsipras alisema hapo jana kwamba sasa ni juu ya viongozi wa Ulaya kutoa jibu. Hata hivyo Kaminsha wa masuala ya uchumi wa Umoja wa Ulaya Pierre Moscovici amesema leo kwamba anao uhakika kuwa Ugiriki itafikia makubaliano juu ya madeni yake na wadai wake wa kimataifa.

Mwandishi:Mtullya Abdu/afpe/ZA

Mhariri:Hamidou Oummilkheir

Hata hivyo Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema makubaliano yanakaribia kupatikana. Lakini Hollande pia aliwaambia waandishi wa habari kwamba kazi kubwa bado inalazimu kufanyika .