1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jumuiya ya ECOWAS yaitaka Ghana kufunguwa mipaka yake kabla marudio ya uchaguzi wa rais

Mohamed Dahman27 Desemba 2008

Jumuiya ya kanda ya Afrika Magharibi hapo jana imekosowa uamuzi wa Ghana kufunga mipaka yake ya ardhini siku mbili kabla ya kufanyika kwa marudio ya uchaguzi wa rais.

https://p.dw.com/p/GNlp
Polisi wa kutuliza ghasia wakiwa macho wakati wa duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais mjini Accra Ghana tarehe 7 mwezi wa Desemba.Picha: AP

Imeitaka serikali ya nchi hiyo kufikiria upya uamuzi wake huo.

Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi wanachama 15 wa mataifa ya Afrika Magharibi ECOWAS imesema katika taarifa kwamba kufungwa kwa mipaka siku mbili kabla ya uchaguzi bila ya taarifa ya kutosha kunatia dosari mchakato wa uchaguzi wa kupigiwa mfano uliojitokeza nchini humo.

Jumuiya hiyo imeitaka serikali ya Ghana kufunguwa tena mipaka yake ya ardhini kwa nia ya ujirani mwema kati ya nchi wanachama wa jumuiya hiyo na kuhakikisha nyendo huru za watu na mtitiriko wa biashara katika eneo hilo halikadhalika kama hatua muhimu ya kuwapa imani miongoni mwa watu.

Mratibu wa usalama wa taifa nchini Ghana Sam Amoo amesema mipaka hiyo itafungwa kuanzia Ijumaa hadi Jumatatu kwa maslahi ya usalama wa taifa.

Ghana inashirikiana mipaka na Togo,Ivory Coast na Burkina Faso.

Marudio ya uchaguzi wa rais wa Ghana hapo kesho yanawakutanisha Nana Akufo - Addo wa chama tawala cha NPP na John Atta-Mills wa chama cha NDC.