Jumuia ya NATO na Mkakati wa Waziri Seehofer Magazetini
11 Julai 2018
Tunaanzia Brussels ulikofunguliwa leo asubuhi mkutano wa viongozi wa jumuia ya kujihami ya NATO. Gazeti la "Trierische Volksfreund" linammulika rais wa Marekani Donald Trump anaehudhuria pia mkutano huo. Gazeti hilo linaandika:" Donald Trump hachoki. Tutegemee kwamba rais huyo wa Marekani atautumia mkutano huo wa jumuia ya kujihami ya NATO ili kuendelea kuishambulia Ujerumani na mataifa mengine wanachama. Na kwa kufanya hivyo haisaidii hata kidogo jumuia hiyo. NATO ni jumuia iliyojengeka kwa misingi ya mshikamano kati ya nchi wanachama. Umoja na mshikamano ndivyo vinavyotangulizwa mbele mkutano kama huu unapoitishwa kila baada ya miaka miwili na sio kupalilia mfarakano. Putin peke yake ndie anaefurahia msimamo ambao si wa busara wa Donald Trump.
Mpango wa kukabiliana na wakimbizi wachapishwa
Waziri wa mambo ya ndani wa serikali kuu ya Ujerumani Horst Sehofer ametangaza baada ya kupita wiki nne, mpango wake wa kimkakati alioupa jina "Mageuzi ya sera ya uhamiaji". Amesema tangu mwanzo mpango huo umeandaliwa na wizara yake na sio serikali kuu ya muungano akishadidia kuwa yaliyomo yameratibiwa kabla ya Julai nne, maridhiano yalipofikiwa pamoja na washirika katika serikali kuu ya muungano.
Maoni ya wahariri yanatofautiana kuhusu mpango huo. Kuna wanaousifu na wengine wanaoukosoa. Gazeti la Oberhessische Presse" linaandika: "CSU wanatumbukiza kila kitu ndani ya chungu kimoja: Wale wanaokimbia vita, wenye kustahiki haki ya kupatiwa kinga ya ukimbizi, wale wanaokimbia umaskini na wahalifu. Eti tunaweza kweli kuwarejesha watu katika nchi inayozongwa na vita? Na ni kwa masilahi ya Ujerumani kweli kumrejesha Afghanaistan kwa mfano mwanafunzi anaesomea kazi ya kuchoma mikate wakati ambapo huku anahitajika? Muhimu wanakataliwa,wanatishwa na kurejeshwa -lakini ndo kusema kwa kila hali? Ikiwa masuala hayo kwenu nyie mlio wengi mnahisi ni sawa, mie naona si sawa."
Umoja ni nguvu
Na hatimae wahariri wameshusha pumzi na kupongeza mshikamano wa kimataifa katika kuokolewa vijana 13 wanasoka waliokuwa wamenasa pangoni nchini Thailand. Wanaleta uwiano na kuokolewa wakimbizi 218 wiki zilizopita katika bahari ya Mediterenia.
Mwandishi:Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Iddi Ssessanga