Jumanne Maalum: Biden aongoza dhidi ya Sanders
4 Machi 2020Seneta Bernie Sanders amenyakua ushindi katika jimbo la nyumbani Vermont, na Colorado, wakati Biden akibeba Minesota, Alabama, Tennessee, Oklahoma, Arkansas na majimbo muhimu ya North Carolina na Virginia. Vituo vya kupiga kura vimefungwa katika majimbo mengi kati ya 14 yanayoshiriki zoezi hilo, lakini upigaji kura unaendelea katika majimbo mawili muhimu sana, Texas na California, kumaanisha kuwa atakayeibuka na ushindi mkubwa kabisa usiku huu bado hajulikani. Ushindi wa makamu wa rais wa zamani Biden katika majimbo hayo yenye Wamarekani weusi wengi umeingiana na ushindi wa mwishoni mwa wiki katika Jimbo la South Carolina.
Sanders anayelemea siasa za mrengo wa shoto alitarajia kupata ushindi rahisi katika jimbo lake la nyumbani, huku akiwanyakua wajumbe 16, lakini Biden mwenye umri wa miaka 77 wa siasa za wastani anataraji kuizuia kasi yake kitaifa – kuanzia Virginia na wajumbe wake 99.
Jumla ya wajumbe 1,357 wanashindaniwa katika uchaguzi huu wa Jumanne Maalum, na Biden anahitaji matokeo mazuri ili kumzuia Sanders kuchukua uongozi mkubwa kabla ya mkutano wa mkuu wa chama utakaomteuwa mgombea wa chama mwezi Julai.
Wengi katika chama cha Democratic wana hamu ya kuizuia kasi ya Sanders katika kura hizi za wajumbe, wakisema seneta huyo atashindwa vibaya kabisa katika uchaguzi mkuu ambao Trump amedokeza kuwa atamuita kuwa msoshalisti anayetaka kuuwekea kikomo mtindo wa maisha ya Wamarekani.
Meya wa zamani wa New York Michael Bloomberg na Seneta wa Massachusetts Elizabeth Warren pia wamo kinyang'anyironi.
Biden ambaye anashiriki katika jaribio la tatu la kuingia Ikulu ya White House baada ya kushindwa katika mwaka wa 1998 na 2008, anaonekana kupata nguvu mpya kutokana na mafanikio yake ya karibuni.
Sanders aliingia katika uchaguzi wa leo akiwa kifua mbele na wajumbe 60n dhidi ya 54 wa Biden katika mapambano ya uteuzi wa jimbo moja hadi jingine.
Sanders yuko mbele ya Biden na mwanya mdogo katika kura za Texas. Umaarufu wa Sanders miongoni mwa Wamarekani wa asili ya Kihispania utampa mavuno katika jimbo hilo, ambako Walatino wanajumuisha thuluthi ya wapiga kura wa Democratic.
Biden, ambaye ushindi wake wa North California umedhihirisha umaarufu wake na wapiga kura weusi, anatumai kushinda majimbo matano ambayo Wamarekani weusi wanajumuisha karibu robo ya wapiga kura wa Democratic: ambayo ni Alabama, North Carolina, Virginia, Tennessee na Arkansas. Majimbo mengine yanayopiga kura leo ni Colorado, Maine, Minnesota, Oklahoma na Utah.
Vimbunga vikali vimeathiri vituo vya kupigia kura katika jimbo la Tennessee wakati hofu ya virusi vya corona ikiviacha baadhi ya vituo vya kupigia kura katika mjimbo ya California na Texas bila wafanyakazi wa kutosha wa uchaguzi.
Vimbunga hiyo vimewauwa watu 25 na kuharibu majengi 140 jimboni humo. Upigaji kura katika jimbo hilo umeongezwa muda kwa saa moja kutokana na changamoto hiyo ya vimbunga.
Watalaamu wa usalama wa taifa waliokusanyika kaskazini mwa jimbo la Virginia katika juhudi isiyo ya kawaida ya uangalizi ili kupambana na mashambulizi ya mitandaoni na upotoshaji wa habari kutoka nje, wamesema uchaguzi huo kufikia sasa haujakumbwa na dalili zozote za kuingiliwa.
Tangu mashirika ya ujasusi ya Marekani yalipohitimisha kuwa Urusi iliingilia uchaguzi wa 2016, serikali ya Marekani imeanzisha hatua za kupambana na udukuzi na shughuli za propaganda ya kigeni zinazolenga kuathiri uchaguzi huo. Urusi imekanusha madai hayo.
Watalaamu wa usalama wa uchaguzi wanasem,a kuwa wakati serikali imefanya maboresho, bado kuna vitisho ambavyo vipo.