1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za muafaka zaanza Zimbabwe

Kalyango Siraj21 Julai 2008

Hatimae Mugabe na Tsvangirai wakaa meza moja

https://p.dw.com/p/EgOt
Morgen Tsvangirai,kushoto na Robert Mugabe,kulia, wasaini hati ya kuanza mazungumzoPicha: AP

Chama cha upinzani nchini Zimbabwe pamoja na chama cha rais Robert Mugabe vimekubaliana kuanza mkakati wa majadiliano ambao una nia ya kumaliza mkwamo wa kisasia ambao umeigubika nchi hiyo kwa mda sasa.

Rais Mugabe wa chama cha ZANU PF pamoja na mpinzani wake Morgen Tsvangira wa chama cha MDC wametia sahihi makubaliano ya kuanza mchakato wa mazungumzo ya kumaliza mkwamo wa kiasa.

Baada ya kutia saini hati hiyo chini ya usimamizi wa rais Mbeki, Morgen Tsvangirai ambae hii ndio mara yake ya kwanza kwa kipindi cha miaka 10 kukaa katika meza moja na Mugabe,amesifu hatua hii.

Nae mpinzani wake rais Mugabe alipewa nafasi kuhutubia waliokusanyika.Alisema kuwa huu ndio mwanzo wa kutafuta njia mpya za kuufumbua mkwamo wa kisiasia pamoja na kiuchumi.

Hati ya makubaliano ya leo jumatatu,miongoni mwa mengine,inataka mazungumzo kufanywa kwa mda wa wiki mbili kuhusu masuala mbalimbali ya mgogoro huo.

Duru za kuaminika zinasema kuwa miongoni mwa masuala hayo ni kuundwa kwa serikali ya umoja pamoja na jinsi ya kuandaa chaguzi zingine.

Mpatanishi mkuu wa mzozo huo,rais wa Afrika Kusini Thabo Mbeki alikuwa mjini Harare kushuhudia tukio hili linalochukuliwa kama la kihistoria na pande zote husika.

Kiongozi wa upinzani Morgen Tsvangirai mwanzo amekuwa akikataa kufanya mkataba wowote na serikali hadi masuala fulani yatimizwe na serikali hiyo.

Miongoni mwa masharti hayo ni kama vile kukomesha ghasia za kisiasa dhidi ya wafuasi wake.Tsvangirai anadai kuwa hadi sasa wameuawa wafuasi wake takriban 120.

Sharti lingine ni kuachiliwa huru wafuasi wake wote walioko kizuizini, kukubali misaada kutolewa tena, na pia kuwaapisha wabunge waliochaguliwa.

Itakumbukwa kuwa MDC ndio ina idadi kubwa ya wabunge katika bunge la sasa la taifa hilo ambalo lilichaguliwa katika uchaguzi uliiopita.

Aidha amekuwa akisisitiza kuwa ni hadi pale rais Mugabe atakapotambua ushindi wake wa duru ya mwanzo uliofanyika Machi29.Lakini taarifa rasmi zilionyesha kuwa japo kashinda lakini kiwango kilikuwa kidogo alichopata kumuwezesha kupata ushindi wa moja kwa moja na ndio maana duru ya pili ikafanyika.

Lakini Tsvangirai alijiondoa dakika za mwisho na hivyo kumpa nafasi Mugabe kupata ushindi wa moja kwa moja.Hata hivyo amekataa kumtambua.

Nacho chama tawala cha ZANU PF kinasema kuwa ni lazima MDC kimtambue Mugabe kama kiongozi halali aliechaguliwa.

Makubaliano haya ya kuanzisha mchakato wa kuzungumzia kwa kina mkwamo huo yalikuwa yatiwe saini wiki iliomalizika lakini Tsvangirai akajiondoa.

Baada ya ushauri wa hapa na pale hatimae MDC kilikubali kutia saini lakini tena kikatoa masharti mengine.Baadhi yalikuwa sherehe hiyo kufanyika katika Harare Hoteli badala ya Ikulu na kutaka sherehe yenyewe iwe ya kiwango cha chini.

Wachambuzi wana sema kuwa hati hii ya kurasa tano haielezei kwa kinaga ubaga uwezekano wa kugawana madaraka,ambao wengine wanaona kama njia pekee kuinusuru Zimbabwe kutoka katika migogoro ya kisaisa na kiuchumi iliyomo.Makubaliano haya ni ya kuupiga jeki mchakato wa mazungumzo.

Vilevile inasemekana kuwa hati hiyo haizungumzii suala nyeti la mustakbala wa Bw Mugabe.

Wachambuzi hao wanaendela kusema kuwa upande wa upinzani ulishawishika kukubali kutia saini makubaliano haya ya hatua ya mpatanishi na mkuu rais Thabo Mbeki kukubali kuwahusisha wadau wengine katika upatanishi huo.Wadau hao ni Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa pamoja na muungano wa mataifa ya kusini mwa Afrika wa SADC.

Na hii ndio mara ya kwanza, kwa kipindi cha miaka 10, kwa Bw Tsvangirai kukaa meza moja na mpinzani wake rais Robert Mugabe.