1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kutafuta chanjo mpya ya Ebola zaanza

Josephat Nyiro Charo5 Februari 2015

Huku mlipuko wa ugonjwa wa Ebola ukianza kupungua Afrika Magharibi, wanasayansi wanatafuta aina mpya ya chanjo zinazohitajika kukabiliana haraka na kikamilifu na mlipuko mwingine unaoweza kutokea.

https://p.dw.com/p/1EVVn
Peking China Ebola Forschung Medizin Helfer Labor
Picha: Imago/Xinhua

Wakati wanasayansi wakiwa wamejizatiti kutopoteza kasi ya utafiti wa kisayansi kuhusu chanjo mpya ya Ebola, watafiti wanasema chanjo hizo, mbali na kuthibitishwa zinafanya kazi, sharti ziwe za bei nafuu, rahisi kuzitumia barani Afrika na ziweze kukabiliana na aina mbalimbali ya virusi. Masharti hayo yanaweza kuwa na maana ya kubadili mbinu za kuvumbua chanjo mpya ambazo zimekuwa zikitumiwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita, lakini haina maana kuwepo taratibu zitakazokwamisha kazi hiyo.

"Tunahitaji akiba ya chanjo kwa sababu kutakuwa na milipuko mingine ya ugonjwa wa Ebola," amesema Seth Berkley, mkurugenzi mtendaji wa Muungano wa Kimataifa wa Chanjo, GAVI, unaosaidia kununua shehena kubwa ya chanjo kwa ajili ya nchi masikini.

Chanjo za majaribio zinazopelekwa sasa Afrika Magharibi zinalenga aina ya kirusi cha Ebola cha Zaire, lakini mlipuko mwingine huenda ukawa tofauti. "Tunahitaji kufanya kazi na sekta ya viwanda vya dawa kutengeza aina ya pili ya chanjo ambayo haitakabiliana tu na kirusi cha Ebola Zaire bali pia Ebola Sudan na pengine kirusi cha Marburg na hata Lassa. Wazo ni kuwa na chanjo itakayofanya kazi katika maeneo mbalimbali," akaongeza kusema Berkley.

Ebola-Impfung in Liberia 02.02.2015
Majaribio ya chanjo ya Ebola LiberiaPicha: John Moore/Getty Images

Liberia imeanza majaribio ya chanjo dhidi ya Ebola Jumatatu wiki hii yanayowajumuisha maelfu ya watu waliojitolea, kama sehemu ya jitihada za kupunguza kuenea kwa ugonjwa huo na kuzuia milipuko katika siku za usoni.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa majaribio hayo naibu waziri wa afya wa nchi hiyo, Tolbert Nyenswah, alisema, "Wakati kazi hii itakapokamilika, Liberia itaingia katika vitabu vya historia kwa kukubali chanjo za majaribio za ugonjwa wa Ebola uliowaua watu zaidi ya 8,000 katika eneo letu. Hii ni safari tuliyoianza na naamini wanasayansi wa pande zote mbili, Liberia na Marekani, wanakaribia kupata suluhisho litakaloyaokoa maisha ya watu siku zijazo."

Wanasayansi wanakabiliwa na changamoto

Kwa sasa wanasayansi wanakabiliana na masuala kadhaa magumu, kwa kiwango fulani kutokana na ufanisi katika kupunguza maambukizi mapya katika mlipuko wa Ebola. Huku kukiwa na maambukizi machache, majaribio makubwa nchini Liberia na Sierra Leone kujaribu chanjo za kwanza za aina moja ya dawa yumkini zisipate idadi kubwa ya takwimu zinazohitajika kuonyesha kama zinafanya kazi.

Na tayari data za awali kutokana na majaribio salama yaliyofanywa kwa binaadamu zinapendekeza chanjo moja kutoka kwa chanjo za kiwango cha juu kutoka kwa kampuni ya GlaxoSmithKline, huenda isichochee mfumo wa ulinzi mwilini kuchangamka kufikia kiwango cha kuweza kuwalinda watu waliokaribiana na kirusi hicho.

Masuala haya pamoja na mengine yanaongeza changamoto na kazi kwa wanasayansi wanaolenga kutengeneza chanjo kwa ajili ya akiba katika siku zijazo. Kutengeneza chanjo ya dawa aina mbili inayoweza kumlinda binaadamu kutokana na aina mbalimbali ya Ebola na magonjwa mengine yanayosababisha kuvuja damu itachukua muda mrefu zaidi, ingawa hata hivyo si jambo lisilowezekana. Baadhi ya chanjo za Ebola zinazofanyiwa majaribio zilianza kama chanjo za dawa kadhaa kabla kubadilishwa kuwa za dawa aina moja kukabiliana na mlipuko wa sasa wa Ebola.

Changamoto nyingine ni kuhakikisha chanjo inaweza kukaa muda mrefu bila kuharibika na iweze kusafirishwa kwa njia rahisi katika nchi za kitropiki. Kwa wakati huu chanjo za majaribio zinahifadhiwa katika mazingira ya nyuzi joto kati ya 70 hadi 80 chini ya sufuri katika kipimo cha Celsius, ingawa kampuni ya Johnson&Johnson inasema chanjo ya Ebola inaweza kuhifadhiwa katika viwango vya joto vya kawaida kwa wiki nyingi.

Symbolbild Baby wird in Sierra Leone geimpft
Mtoto akidungwa chanjo ya Ebola Sierra LeonePicha: , Francisco Leong/AFP/Getty Images

Hatimaye kampuni zinahitaji kupata idhini kutoa ushahidi wa wazi kabisa kwamba chanjo ziko salama na zinafanya kazi kwa binaadamu, jambo ambalo ni changamoto wakati majaribio makubwa yanaposhindwa kupata matokeo yaliyotarajiwa.

Watafiti na watengezaji madawa wanasema maafisa wa kudhibiti viwango wameashiria chanjo za Ebola huenda zikaidhinishwa kwa kutumia data kutoka kwa majaribio yaliyofanyiwa tumbili na wanyama wengine mbali na binaadamu, pamoja na ushahidi kwamba ziko salama na zinasaidia kuimarisha mfumo wa ulinzi katika mwili wa binaadamu, hivyo kutoa muelekeo kuhusu mipango kabambe ya chanjo zinazonuiwa kukabiliana na mashambulizi ya kigaidia kutumia viumbe hai.

Kituo cha utafiti chazinduliwa Berlin

Akizungumza Jumanne wiki hii wakati wa uzinduzi wa kituo cha utafiti wa virusi vinavyosababisha magonjwa yanayofanana na Ebola katika taasisi ya Robert Koch, mjini Berlin, kansela wa Ujerumani Angela Merkel alisema mengi yanapasa kufanywa kuzuia mlipuko wa magonjwa ya kuambukizwa.

Merkel aidha alisema, "Katika kipindi kirefu sisi na ulimwengu wote kwa jumla tunatakiwa tujiandae vyema zaidi dhidi ya mlipuko wa magonjwa kama Ebola. Ni muhimu sana kujifunza kutokana na tuliyoyashuhudia yakitokea kwa sababu ya Ebola. Tayari kuna mapendekezo, lakini sasa kuna haja ya kuyachunguza na kuchagua yanayofaa kwa ufanisi wa kuonekana."

Mwandishi:Josephat Charo/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman