Juhudi za kupambana na virusi vya Corona zapamba moto Ulaya
3 Aprili 2020Hatua za kupambana na maambukizi ya virusi vya corona zinaendelea mnamo wakati shehena za madawa, vifaa vya kujikinga na mashine za kusaidia kupumua vikiendelea kuwa haba kila muda unavyokwenda.
Wimbi la vifo vinavyotokana na virusi vya corona pamoja na kupotea kwa nafasi za ajira limeikumba Marekani na Ulaya. Kiasi ya wamarekani milioni 10 wametupwa nje ya ajira katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, ikiwa ni kuporomoka kwa kushangaza kabisa nchini Marekani kwa soko la kazi hali ambayo haijawahi kushuhudiwa. Duniani kote watu waliothibitika kuambukizwa virusi vya corona wamepindukia milioni moja na vifo vimefikia watu 53,000, kwa mujibu wa idadi iliyokusanywa na chuo kikuu cha Johns Hopkins.
Mahospitali katika jimbo la Catalonia nchini Uhispania likiwa jimbo la pili nchini humo kuathirika na maambukizi ya janga la virusi vya corona, yako katika hali mbaya ya kuelemewa, kiongozi wa jimbo hilo Quim Torra ameliambia shirika la habari la Reuters leo.
Jimbo hilo la pili nchini Uhispania kwa idadi ya wakaazi ina idadi kubwa ya wagonjwa wa virusi vya corona katika kiwango cha wagonjwa mahututi wanaofikia 2,053, kwa mujibu wa data za hivi karibuni, na imewaorodhesha watu 2,335 waliofariki, ikiwa ni ya pili kwa vifo baada ya mji mkuu Madrid.
Hatua zilizotumika hapa Ujerumani kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona zina matokeo chanya kiasi, lakini ni mapema mno kusema kila kitu ni shwari, shirika la serikali la udhibiti wa magonjwa limesema leo.
Boris Johnson kubakia nyumbani
Kwa siku chache zilizopita hadi sasa, mtu mmoja aliyeambukizwa na virusi vya corona nchini Ujerumani, amekuwa kwa wastani akimuambukiza mtu mmoja mwingine , kwa mujibu wa taasisi ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch. Wiki moja iliyopita , idadi hiyo ilikuwa mtu mmoja anawaambukiza watu watano, ama hata saba. Lakini data hizo mpya hazileti uhalali wa kuwa kila kitu ni shwari, amesema Lotha Wieler rais wa taasisi hiyo ya Robert Koch.
Waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema leo kuwa ataendelea kujitenga baada ya kuthibitika kuwa na virusi vya COVID-19, kufuatia wiki moja ya kubakia nyumbani na kufanyakazi akiwa huko.
Wachuuzi wa kando kando ya barabara wakivalia vifaa vya kujifunika pua na mdomo pamoja na glovu mikononi walionekana wakiuza bidhaa mbali mbali pamoja na nyanya, karoti na mboga nyingine na nyama ya nguruwe kwa wanunuzi leo Ijumaa katika mji wa Wuhan ambao ndio kitovu kilichoanzia ugonjwa huu wa virusi vya corona., wakati wafanyakazi wanajitayarisha kwa ajili ya kumbukumbu ya kitaifa mwishoni mwa juma kwa wafanyakazi wa sekta ya afya na wengine waliofariki kutokana na kuzuka kwa virusi hivyo.
Nchi tatu za Afrika zimetoa taarifa ya mapema kuwa janga la corona limeharibu uwezekano wa ukuaji wa uchumi wao mwaka huu. Burkina Faso jana ilipunguza matarajio yake ya ukuaji wa pato jumla la taifa , GDP kwa mwaka 2020 kutoka asilimia 6.3 hadi asilimia 2, katika hotuba ya taifa aliyotoa rais Roch Kabore.
Cote d'Ivore ilikuwa nchi ya kwanza kufanya hivyo siku ya Jumanne kwa kusema makadirio yake yamepunguzwa kwa nusu kutoka asilimia 3.6.