1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kimataifa kutafuta chanjo ya corona zaendelea

25 Aprili 2020

Umoja wa Mataifa umezindua juhudi za kimataifa za kutafuta chanjo ya virusi vya corona, wakati Rais wa Marekani Donald Trump akizusha mjadala kwa kudai kuwa wagonjwa watibiwe na kemikali za kuuwa vijidudu

https://p.dw.com/p/3bO5E
Coronavirus - Virus SARS-CoV-2
Picha: picture-alliance/dpa/Niaid/Europa Press

Hayo yanajiri wakati idadi ya vifo nchini Marekani ikipindukia 50,000. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kulitatua janga hili kutahitaji mashirika ya kimataifa na viongozi wa ulimwengu kuungana na sekta ya kibinafsi kutengeneza na kusambaza chanjo ya virusi vya corona.

Ombi hilo la mkuu wa Umoja wa Mataifa lilikuja siku moja baada ya rais wa Marekani Donald Trump kusababisha ukosoaji mkubwa kutokana na pendekezo lake kuwa kemikali za kuuwa vidudu zitumike kuwatibu wagonjwa.

"Kuna njia yeyote tunaweza kufanya kitu kama hicho, kwa kuingiza kemikali hizo mwili kwa kutumia shindano au kama kusafisha?" Trump alisema wakati wa kikao cha habari. "Inaonekana kuwa kitu cha kupendeza kwangu"

Symbolfoto Impfstoff
Wanasayansi duniani wanafanya majaribio ya chanjo Picha: picture-alliance/Geisler-Fotopress/C. Hardt

Wakati watalaamu – na kampuni za kutengeneza kemikali za kuuwa vijidudu – wakijitoa waziwazi haraka kuonya dhidi ya majaribio yoyote hatari ya aina hiyo, rais huyo alijaribu kuzifuta kauli hizo kwa kudai kuwa alikuwa akizungumza kama kejeli.

Kufikia jana Ijumaa, visa vya virusi vya corona vilifikia milioni 2.77 kote duniani, huku kukiwa na vifo 193,930.

Mjini Geneva, shirika la Afya Ulimwenguni – WHO lilifanya mkutano wa video kuhusu ushirikiano wa kimataifa wa kutengeneza chanjo, pamoja na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, Wakfu wa Gates na GAVI, ambao ni muungano wa kimataifa wa utoaji chanjo.

Guterres aliwaambia viongozi hao kuwa ulimwengu unahitaji kuona utafiti, utengenezaji na usambazaji kwa njia ya usawa na mwafaka wa chanjo za COVID-19, pamoja na vifaa vya matibabu.

Katika ulimwengu wa Kiarabu, mamia kwa mamilioni ya waumini waliufungua mwezi mtukufu wa Ramadhan chini ya masharti ya kubakia majumbani, wakikabiliwa na marufuku ya kufanya maombi misikitini na utamaduni wa mikusanyiko mikubwa ya familia na marafiki saa za jioni. 

UN Covid-19 Virtuelle Pressekonferenz António Guterres
Umoja wa Mataifa unahimiza kupatikana kwa chanjoPicha: webtv.un.org

Watalaamu wawaambia Wajerumani waendelee kubakia majumbani

Nchini Ujeurumani, Taasisi ya afya ya umma ya Robert Koch - RKI imeonya dhidi ya hatua ya kuondoa vizuizi kwa wingi, wakati majimbo mengi ya shirikisho yakiondoa agizo la kudhibiti usafiri wa watu.

Onyo hilo limekuja wakati uchunguzi mpya wa maoni wa shirika la utangazaji la ZDF ukionyesha kuwa asilimia 55 ya Wajerumani wanaunga mkono mpango wa kuondolewa taratibu hatua za kusitishwa shughuli za kila siku ulioanza kutekelezwa wiki hii katika baadhi ya majimbo. RKI imesema jana kuwa idadi ya visa vilivyothibitishwa vya virusi vya corona nchini Ujerumani itahitaji kupungua hadi katika mamia ya watu kwa siku, kabla ya nchi hiyo kuzingatia kulegeza vikwazo.

Kufikia jana, Ujerumani ilikuwa na visa vipya 2,337, ikiwa ni idadi ya chini ikilinganishwa na siku tatu zilizopita mfululizo. Katika makubaliano kati ya serikali kuu na majimbo, maduka yasiyo ya bidhaa muhimu yenye ukubwa wa mita 800 za mraba yalifunguliwa upya, pamoja na biashara ya magari, maduka ya vitabu na baiskeli.