Juhudi za kidiplomasia Misri zaendelea
5 Agosti 2013Wanadiplomasia hao walikutana na naibu kiongozi wa udugu wa kiislamu Khairat El Shater saa sita usiku, baada ya kupewa ruhusa na mwendesha mashitaka mkuu wa Misri kumtembelea kiongozi huyo katika jela ya Tora iliyoko kusini mwa mji wa Cairo.
Shirika la habari la serikali ya Misri MENA limeripoti kuwa ziara hiyo iliwajumuisha maafisa kutoka Marekani,umoja wa ulaya,jumuiya ya falme za kiarabu na Qatar na kunukuu duru za kuaminika.Hapo awali serikali ya Misri ilikuwa imekanusha kuwa maafisa hao waliruhusiwa kumuona El shater.
Kiongozi wa ududgu wa kiislamu atambelewa jela
El Shater ambaye ni naibu kiongozi wa udugu wa kiislamu,kundi ambalo lilikandamizwa kwa miongo mingi na kuibuka baada ya Hosni Mubarak kung'olewa madarakani na kumsaidia Mursi kushinda katika uchaguzi mkuu wa kwanza huru nchini humo mwaka jana,anaonekana kuwa mpangaji mikakati mkuu wa masuala ya kisiasa wa kundi hilo na alikamatwa baada ya Mursi kupinduliwa na jeshi madarakani wiki tano zilizopita.
Juhudi za upatanishi za kimataifa zinasaidia kudhibiti hali na kuzuia umwagikaji wa damu kati ya wafuasi wa Mursi na serikali ya muda iliyowekwa madarakani na jeshi lililoipindua serikali ya Mursi.
Serikali hiyo ya muda siku ya Jumamosi ilisema itaupa upatanishi nafasi lakini ikaonya muda unayoyoma wa kufanya hivyo.Maelfu ya wafuasi wa Mursi bado wamekita kambi katika maeneo mawili mjini Cairo huku serikali ikitangaza kuwa maandamano hayo ni tishio kwa usalama wa kitaifa na kuapa kuwatawanya.
Viongozi wa kiislamu wafunguliwa mashitaka
Hapo jana mahakama moja mjini Cairo ilitangaza kuwa kiongozi wa udugu wa kiislamu Mohammed Badie na manaibu wake wawili El-Shater na Rashid Bayoumi watafikishwa mahakamani tarehe 25 mwezi huu kwa mashitaka ya uchochezi na mauaji wakati wa maandamano yaliyomng'oa madarakani Mursi.
Hatua hiyo ya mahakama huenda ikatatiza juhudi za kutafuta mchakato wa kisiasa,kuhimiza maridhiano ya kitaifa na kuepusha umwagikaji wa damu.Serikali ya muda imesema inataka maridhiano hayo kujumuisha udugu wa kiislamu lakini imesema sharti kundi hilo kwanza lilaani na kusitisha ghasia.
Wakati wa mkutano na naibu waziri wa mambo ya nje wa Marekani William Burns na mjumbe wa umoja wa ulaya Bernadino Leon siku ya Jumamosi,ujumbe wa wafuasi wa Mursi ulisema uko tayari kuzungumza na wanasiasa waliounga mkono kuondolewa madarakani kwa mursi lakini pia wakataka kurejeshwa kwa katiba iliyofutiliwa mbali na kutaka jeshi kujitenga na siasa.
Rais wa Marekani Barrack Obama amewataka maseneta Lindsey Graham na John McCain kusafiri Misri kuktuana na viongozi wa serikali ya muda na wa upinzani.Graham amesema jeshi haliwezi kuendelea kuliendesha taifa hilo kwani kinachohitajika ni chaguzi za kidemokrasia.
Mwandishi:Caro Robi/Reuters/Dpa
Mhariri: Gakuba Daniel