1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo juu ya nyuklia ya Iran katika hatua mwisho

Admin.WagnerD31 Machi 2015

Juhudi za dakika za mwisho zinafanyika mjini Lausanne ili kufikia makubaliano juu ya mpango wa nyuklia wa Iran. Wajumbe kwenye mazungumzo wanao muda wa hadi usiku wa manane lakini bado pana tafauti kubwa

https://p.dw.com/p/1Ezyc
Mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran mjini Lusanne
Mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia mjini LusannePicha: Reuters/B. Smialowski

Wajumbe wa kibalozi wamo mbioni katika juhudi za kuutatua mgogoro wa nyuklia wa Iran. Wajumbe wa nchi ambazo ni wanachama wa kudumu kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani wanapaswa kupatana na wajumbe wa Iran juu ya mpango wa nyuklia wa nchi hiyo hadi itakapofikia usiku wa manane leo lakini wachunguzi wanasema tafauti, kubwa bado zipo baina ya pande hizo mbili. Wachunguzi hao wamesema huenda mapatano yakapatikana au yasipatkane.

Hatahivyo Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov ameseme leo kuwa anapanga kurejea tena kwenye mazungumzo mjini Lausanne na ametamka kwamba mambo siyo mabaya. Lavrov hata amewaambia waandishi wa habari mjini Moscow kuwa matarajio ni mazuri. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier naye amesema kuwa mazungumzo juu ya mpango wa nyuklia wa Iran yameingia katika hatua muhimu sana.

Waziri John Kerry akiwa na Javad Zarif wa Iran.
Waziri John Kerry akiwa na Javad Zarif wa Iran.Picha: Reuters/Brian Snyder

Bora mapatano yoyote kuliko kuondoka mikono mitupu

Naye Mbunge wa chama cha Kijani nchini ´Ujerumani Omid Nouripour ambae pia ni msemaji wa masuala ya nje wa chama hicho ameeleza matumaini ya kupatikana suluhisho kwenye mazungumzo ya mjini Lausanne. Amesema anatumai sana mapatano yatafikiwa. Amesema bora kupatana kwa namna fulani kuliko kuondoka mikono mitupu.

Bado pana utatanishi kwenye mazungumzo

Lakini bado yapo masuala ya utatanishi na hasa ya kisiasa yanayopaswa kuzingatiwa kwenye mazungumzo ya mjini Lausanne. Iran inataka vikwazo ilivyowekewa na jumuiya ya kimataifa , viondolowe haraka na pia iruhusiwe kuendelea na mpango wake wa kinykulia bila ya vizingiti vyovyote.

Kwa upande wao mataifa yanayofanya mazungumzo ya Iran yanataka vikwazo vilivyowekwa na Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran vinavyohusu kuhamisha tekinolojia ya kiatomiki viendelee kuwekwa kwa muda mrefu kwa kadri itakavyowezekana.

Waziri Javad Zarif akisubiri kuanza kwa mkutano katika hoteli mjini Lausanne.
Waziri Javad Zarif akisubiri kuanza kwa mkutano katika hoteli mjini Lausanne.Picha: picture-alliance/AP Photo/Smialowski

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amemwambia ripota wa shirika la televisheni la Marekani CNN kwamba kila mtu anautambua umuhimu wa leo. Waziri Kerry amesema bado yapo masuala ya utatanishi.

Waziri huyo wa Marekani amekuwa anakutana na Waziri wa mambo ya nje wa Iran, Mohammed Javad Zarif mjini Lausanne tokea Alhamisi ya wiki iliyopita. Mawaziri hao wamekuwa wanafanya mazungumzo ya undani katika juhudi za kuyafikia mapatano yatakayoweka msingi wa kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia.

Iran tayari kupunguza kurutubisha Uran

Waziri Kerry na wajumbe wengine wa mataifa muhimu wanaofanya mazungumzo na Iran wamesema hatua imepigwa kwenye mazungumzo hayo kutokana na Iran kukubali kuyazingatia matakwa ya upande mwingine juu ya kupunguza zaidi kiwango cha kuyarutubisha madini ya Uran katika mpango wake wa nyuklia.

Mwandishi: Mtullya Abdu./afpe,rtre/ZA
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman