1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi mpya za kuunda serikali ya kisiasa Italia

Daniel Gakuba
30 Mei 2018

Vyama vikuu nchini Italia vimefufua juhudi za kuunda serikali ya mseto, ili kumaliza mkwamo wa kisiasa unaoendelea nchini humo baada ya uchaguzi wa mwezi tarehe 4 Machi ambao haukubainisha mshindi wa wazi.

https://p.dw.com/p/2yeop
Der designierte PM Cottarelli trifft Präsident Mattarella - Rom
Picha: picture-alliance/abacapress

 

Vyama vilivyoongoza kwa kura nyingi katika uchaguzi uliopita wa Machi 4 vinajaribu kuafikiana juu ya jina la mtu mwingine atakayeteuliwa kushika wadhifa wa waziri wa uchumi katika serikali yao ya mseto, baada yule wa awali, Paolo Savona kukataliwa na Rais Sergio Mattarella, na kuvifanya vyama hivyo, Vuguvugu la Nyota Tano na League kuachana na mpango wa kuunda serikali ya kuiongoza nchi. Hii ni kwa mujibu wa chanzo cha habari kilicho karibu na Vuguvugu la Nyota tano aliyenukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Uwezekano huo umedokezwa na Waziri Mkuu mteule Carlo Cottarelli, alitwishwa na rais jukumu la kuunda serikali ya mpito kuelekea uchaguzi mpya ambao uunapangwa kufanyika Julai 29. Cottarelli amenukuliwa na shirika la habari la Italia, ANSA, akisema kumeibuka uwezekano mpya wa kupatikana kwa serikali ya kisiasa, akimaanisha kuwa uwezekano wa serikali inayoongozwa na mwanasiasa, badala ya ile iliyo chini ya mtalaamu kama yeye.

Cottarelli ambaye amefanya mashauriano na rais, amesema hali halisi ya mambo, hususan wasiwasi mkuba katika masoko ya fedha na mitaji, imemfanya kusubiri maendeleo mapya.

Uchunguzi wa maoni wakipa kichwa chama cha League

Rom Matteo Salvini Chef Lega Nord
Matteo Salvini, kiongozi wa chama cha LeaguePicha: Reuters/T. Gentile

Lakini wakati hayo yakijiri, Mateo Salvini, kiongozi wa chama cha League ambacho kulingana na uchunguzi wa maoni kinazidi kupata umaarufu, ameonekana kupuuza dhana hiyo ya serikali kati ya chama chake na Vuguvugu la Nyota Tano, akisisitiza haja ya kufanyika uchaguzi mpya haraka inavyowezekana.

Amesema na hapa namnukuu, ''Nilikuwa mjini Roma kwa wiki kadhaa tukijaribu kuunda serikali, lakini juhudi zetu ziliambulia patupu. Sasa, narejea kwa umma wa Italia, kile ambacho walituzuia kukifikia waiki iliyopita, tutakipata kupitia kura za mamilioni ya watu mnamo miezi miwili au mitatu ijayo.''

Licha ya hayo lakini, Salvini alioneka kuunga mkono kuundwa kwa serikali ya mpito kuongoza kwa muda mfupi, akisema uchaguzi wa mwishoni mwa mwezi Julai unaweza kuvuruga shughuli za watu wenye vibarua vya muda mfupi.

Bunge ni kizingiti kwa Cottarelli

Italien Rom Carlo Cottarelli mit Regierungsbildung beauftragt
Carlo Cottarelli, Waziri Mteule wa Italia Picha: picture-alliance/NurPhoto/S. Lore

Waziri Mkuu wa mpito aliyeteuliwa na rais, Carlo Cottarelli, wakati huu hana uungwaji mkono wa kutosha bungeni, hata wa kumruhusu kuunda serikali hiyo iliyokusudiwa kuongoza hadi tarehe ya uchaguzi mpya.

Taarifa hizo za uwezekano wa kupatikana kwa serikali ya kisiasa na hivyo kumaliza mkwamo wa uongozi zimeleta ahueni katika masoko ya fedha na mtaji. Ahueni hiyo imepewa msukumo na tangazo la Benki Kuu ya Ulaya, ambaye imesema kuwa ingawa inafuatilia kwa makini yanayoendelea Italia, bado haijaona sababu ya kuingilia kati.

Chanzo kutoka benki hiyo yenye makao yake mjini Frankfurt Ujerumani, kimesema mzozo wa Italia haujafika kiwango cha kutishia akiba ya mabenki, na kuongeza kuwa benki ya Ulaya inatumai kitisho hicho hakitajitokeza siku za usoni.

Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, dpea

Mhariri: Grace Patricia Kabogo