1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jubilee nayo yataka mfumo mbadala wa kura

6 Juni 2017

Sasa chama cha Jubilee cha Rais Uhuru Kenyatta nacho kinataka mfumo wake mbadala wa kukusanyia matokeo ya kura za urais kama muungano wa NASA wa hasimu wake, Raila Odinga, kinyume na msimamo wake wa awali.

https://p.dw.com/p/2eAJJ
Kenia Wahlen Uhuru Kenyatta und William Ruto
Picha: Reuters

Awali chama hicho kilikuwa kinapinga upinzani na kuishinikiza Tume Huru ya Mipaka na Uchaguzi (IEBC) isiruhusu vyama kuwa na mifumo yao mbadala ya kuhesabu matokeo ya kura.

Lakini wakati rufaa ya IEBC kupinga kutangazwa kwa matokeo ya kura ya urais inasikizwa leo, jitihada za Jubilee kuwa na mfumo wake inatajwa kuwa ishara ya juhudi za Rais Kenyatta kuhakikisha kuwa haongozi kwa kipindi kimoja tu.

Hiyo inamaanisha kuwa sasa ni bayana kuwa kutakuwa na mifumo mitatu sambamba ya kuhesabia kura za urais kwenye uchaguzi mkuu  wa Agosti 8, ambapo chama tawala, Jubilee, kinajiunga na IEBC na muungano mkuu wa upinzani, NASA, ambao tayari umeshafanya hivyo.

Vitengo vya mfumo huo vinajumuisha kamati ya kiufundi, washauri wa mikakati, washauri wa siasa, wataalamu wa masuala ya mawasiliano na makundi ya vijana na kinamama katika viwango vya mashinani.

Ingawa hapo awali vinara wa chama hicho, akiwemo Makamu wa Rais William Ruto, walikuwa wakikosoa vikali mipango ya upinzani ya kuwa na mfumo sambamba wa kuhesabia kura kwa madai kuwa ni kichocheo cha ghasia baada za uchaguzi mkuu, lakini sasa kamati ya mkakati ya Rais Kenyatta imekutana kujadili mbinu za kukabili mipango ya upinzani.

NASA waapa kuendelea kukusanya matokeo wenyewe

Protest in Kenia Raila Odinga 07.07.2014
Vinara wa Muungano wa NASA unaoongozwa na Raila Odinga (katikati) wanasema mfumo mbadala wa kukusanyia matokeo ya kura ni muhimu kwao.Picha: SIMON MAINA/AFP/Getty Images

Muungano mkuu wa upinzani, NASA, umekuwa ukiweka mikakati ya kuzuia wizi wa kura kwa kuweka kamera katika vituo vyote 41,000 vya kupiga kura kabla ya uchaguzi mkuu wa hapo Agosti. Kiongozi mkuu wa muungano huo, Raila Odinga, anasema hatua hiyo ni mwafaka katika kuwahakikishia wanapata ushindi.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema kuwepo kwa mifumo mingi ya kutangaza matokeo ya urais huenda kukasababisha hali ya suintafahamu nchini Kenya.

IEBC yaenda mahakamani kupinga 

Huku hayo yakijiri, rufaa ya IEBC kupinga matangazo ya kura ya urais katika majimbo inasikizwa leo, kwa mujibu wa mwenyekiti wa tume hiyo, Wafula Chebukati. 

Kwa mujibu wa sheria za sasa za uchaguzi, ni IEBC  pekee yenye haki ya kutangaza matokeo ya kura za urais.

Vile vile, IEBC imemfuta kazi mkurugenzi wake wa uuzaji na ununuzi, Lawy Aura, kwa kuchelewa kuleta karatasi za kupiga kura miezi miwili kabla ya uchaguzi huo mkuu, hatua inayoibua swali iwapo tume hiyo iko tayari kuendesha uchaguzi mkuu tarehe 8 Agosti.

Mwandishi: Shisia Wasilwa/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef