JUBA : Waasi wa LRA watakiwa kuondoka Sudan kusini
9 Februari 2007Gavana wa jimbo la kusini mwa Sudan amewaamuru waasi wa LRA wa Uganda wanaoishi kusini mwa Sudan kuondoka kwenye jimbo hilo.
Kundi moja la waasi wa LRA lilikuwa limeruhusiwa kubakia kusini mwa Sudan karibu na mpaka na Uganda chini ya makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano yaliofikiwa na serikali ya Uganda na wapatanishi wa kusini mwa Sudan wakati mazungumzo ya amani yakiendelea katika mji wa Juba.
Gavana wa jimbo hilo Aleisio Ojetuk ameliambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba kutokana na waasi hao kugoma kurudi kwenye mazungumzo ya amani hakuna sababu ya kuendelea kubakia hapo na kwamba wanapaswa kuondoka.
Kundi jengine ukiwemo uongozi wa juu inaaminika kuwa limepiga kambi kwenye mpaka wa Sudan na Congo.
Mazungumzo hayo ya amani yalikwama mwezi uliopita baada ya waasi kusema kwamba hawatoendelea tena na mazungumzo mjini Juba kutokana na kuhofia usalama wao baada ya Rais Omar Hassan al Bashir wa Sudan kutishia kuwatokomeza waasi wa LRA kutoka Sudan.
Waasi hao wamesema wanataka mahala pengine kufanyia mazungumzo hayo aidha Kenya au Afrika Kusini lakini katu hawatofanya mazungumzo hayo nchini Sudan.