1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Kerry kuwa waziri wa mambo ya nje?

Abdu Said Mtullya22 Desemba 2012

Rais Obama ametangaza amemteua John Kerry kuwa Waziri wa mambo ya nje ajae. Ikiwa atathibitishwa, Seneta huyo wa Massachusetts atachukua nafasi ya Waziri wa sasa Bibi Hillary Clinton

https://p.dw.com/p/177py
Seneta John Kerry ateuliwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani
Seneta John Kerry ateuliwa Waziri wa mambo ya nje wa MarekaniPicha: Reuters

Rais Obama amemwita Kerry kuwa mtu anaefaa kuziongoza sera za nje za  Marekani katika miaka ijayo.

Kerry mwenye umri wa miaka 69 alitajwa kuwa anaefaa kuushika wadhifa huo baada ya balozi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa Susan Rice wiki iliyopita kujitoa kwenye kinyang'anyiro cha kuuwania.

Balozi Rice alichukua hatua hiyo kutokana na kusakamwa kwa lawama  za wajumbe wa chama cha Republican kuhusiana na mashambulio yaliyofanywa kwenye ubalozi mdogo wa Marekani mjini Beghazi nchini Libya mapema mwaka huu.Watumishi kadhaa waliuawa .

Rais Obama amesema maisha yote ya John Kerry yamemtayarisha kwa ajili ya kazi hiyo. Obama alitoa mfano wa kazi aliyoifanya Kerry katika jeshi la majini la Marekani wakati wa vita vya Vietnam. Na pia kazi ya useneta aliyoifanya kwa karibu miaka karibu 30.

Obama alieleza sababu ya kumteua Kerry kuchukua nafasi ya Hillary Clinton.Amesema mwanasiasa huyo ametoa mchango mkubwa katika sera za nje  za Marekani juu ya masuala ya Aghanistan,Pakistan na katika juhudi za kurejesha uhusiano wa kibalozi baina ya Marekani na Vietnam. Obama ameusifu mchango mkubwa wa Seneta John Kerry katika sera za nje za Marekani, kutokana na kazi aliyofanya kama mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa nje.

Hillary Clinton amsifu Kerry:

Waziri wa mambo ya nje wa sasa Hillary Clinton pia amesema John Kerry amepitia mitihani ya vita,serikali na diplomasia.Na wakati wote amethibitisha uwezo wake. Katika tamko, Waziri Clinton amemwita Kerry kuwa mtu anaefaa kwa kazi ya  kuongoza sera za nje za Marekani.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary Clinton
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Hillary ClintonPicha: dapd

John Kerry aliachana na ndoto ya kuwania Urais baada ya kushindwa kwa kura chache na George Bush wa chama cha Republican katika uchaguzi wa Rais uliofanyika mnamo mwaka wa 2004 nchini Marekani. Lakini alijijengea utambulisho mpya kama kiongozi wa mahusiano ya nje kwenye bunge na kuwa muungaji mkono mkubwa wa Rais Obama.

Akianza kazi,Kerry ambaye amekuwa Seneta wa jimbo la Massachusetts mara tano, atakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa pamoja na mgogoro wa Syria,mpango wa nyuklia wa Iran na uhusiano baina ya Marekani na Urusi na China.

Kerry anatarajiwa kuthibitishwa na bunge.Hata wajumbe wa chama cha Republican wanatumai kuwa Kerry atapita katika mchakato wa kuthibitishwa kuwa Waziri wa mambo ya nje wa Marekani. 

Mwandishi: Mtullya Abdu./RTRE

Mhariri: George, Stumai