1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

John Kerry afanya mazungumzo Berlin

Elizabeth Shoo22 Oktoba 2014

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani na mwenzake wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeier, walitembelea kumbukumbu ya ukuta wa Berlin ulioangushwa miaka 25 iliyopita. Kerry anakutana pia na Merkel.

https://p.dw.com/p/1DZwf
John Kerry na Frank-Walter Steinmeier
Picha: Reuters/Brian Snyder

Kwa John Kerry, mji wa Berlin ni sehemu ya historia yake binafsi. Alipokuwa mtoto aliishi na wazazi wake katika mji mkuu wa Ujerumani kwa miaka kadhaa. Yeye na waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier leo waliweka mashada kwenye kumbukumbu ya ukuta wa Berlin. Akizungumza kwa Kijerumani, Kerry alisema kuwa mgawanyiko wa nchi hii usingeweza kuhitimishwa bila ya msaada kutoka Marekani. Kerry alisisitiza kuwa nchi hizo mbili bado ni washirika wa karibu. "Ujerumani na Marekani kwa muda mrefu zimeshirikiana kuleta uhuru, amani na maisha bora. Nafurahi sana kuwa hapa na kuimarisha uhusiano wetu na Ujerumani," alisema Kerry.

Hata hivyo, uhusiano huo uliyumbishwa na kashfa ya udukuzi unaofanywa na mashirika ya kijasusi ya Marekani kwa raia na wanasiasa wa Ujerumani.

Kwa upande wake, Steinmeier alionya kwamba mgogoro unaoendelea Ukraine unatishia amani kwa mataifa mengine ya Ulaya. Alisema umoja wa Ukraine kwa sasa upo hatarini. "Ndio maana ni wajibu wetu kuzuia mgawanyiko mpya kutokea barani Ulaya."

Merkel asifu ushirikiano

Steinmeier aliwataka pia rais Vladimir Putin wa Urusi na mwenzake Petro Poroshenko wa Ukraine kuheshimu makubaliano ya amani yaliyofikiwa katika mji mkuu wa Belarus, Minsk.

Kerry na Steinmeier waliweka mashada kwenye kumbukumbu ya ukuta wa Berlin
Kerry na Steinmeier waliweka mashada kwenye kumbukumbu ya ukuta wa BerlinPicha: Pool/Getty Images

Mada nyingine walioizungumzia Steinmeier na Kerry ni tishio la kundi linalojiita Dola la Kiislamu. Steinmeier alisema nchi yake na Marekani zilifanya jambo sahihi zilipoamua kuwaunga mkono wapiganaji wa Kikurdi wanaopambana na waasi wa IS.

Kabla ya Kerry kufanya mazungumzo na Angela Merkel, kansela huyo wa Ujerumani aliusifu ushirikiano wa karibu baina ya nchi yake na Marekani. Merkel alisisitiza umuhimu wa Ujerumani na Marekani kujadiliana kabla ya kukubaliana hatua za kuchukua kwenye matukio ya kimataifa, kama vile mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu au namna ya kuudhibiti ugonjwa wa Ebola.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/afp/dpa

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman