JOHANNESBURG : UKIMWI unauwa mtoto kila dakika 15 Zimbabwe
18 Machi 2005UNICEF imesema UKIMWI unauwa mtoto nchini Zimbabwe kila baada ya dakika 15 na imetaka wafadhili duniani kufunguwa mifuko yao ya fedha kupiga vita janga hilo nchini humo kwa nguvu ile ile inayotumika kugombania demokrasia.
Carol Bellamy akiwa katika safari yake ya mwisho barani Afrika kama Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Shirika Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuwahudumia Watoto ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Johannesburg kwamba Zimbabwe inapokea sehemu ndogo ya fedha ikilinganishwa na nchi nyengine katika eneo hilo licha ya kuathirika vibaya kotokana na kuwa na kiwango kikubwa sana cha virusi vya HIV na UKIMWI duniani pomoja na kuongezeka kwa idadi ya vifo vya watoto.
Amesema wafadhili wamechukuwa msimamo mkali kwa Zimbabwe juu ya masuala ya utawala bora lakini watoto wasiokuwa na hatia wamekuwa wakiteseka kama matokeo hayo.
Bellamy ambaye anamaliza muda wake hapo mwezi wa Juni baada ya kutumikia wadhifa huo wa Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa kutetea watoto kwa miaka 10 amesema dunia lazima itafautishe kati ya siasa na Zimbabwe.