JOHANNESBERG:Askofu wa kikatoliki Zimbabwe amshutumu Mugabe
11 Julai 2007Kiongozi mmojawapo wa kanisa katoliki nchini Zimbabwe amemkosoa rais Mugabe akisema hana mwelekeo juu ya kutatua tatizo la mfumko mkubwa wa bei nchini humo.
Akizungumza kutoka mjini Johannesberg Afrika kusini askofu mkuu wa Bulawayo Pius Ncube amemtaja kiongozi huyo wa Zimbabwe kuwa mzee anayenga’ngania madaraka licha ya chama chake kumrai ajiuzulu.
Matamshi hayo ya Askofu Ncube yamekuja wakati hali ya maisha inazidi kuwa mbaya nchini Zimbabwe.
Aidha kiongozi huyo wa kidini ametoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa iongeze shinikizo dhidi ya Mugabe kukabiliana na janga hilo.
Hata hivyo amesisitiza kuwa hawezi kuunga mkono hatua ya kupelekwa jeshi la nje kwa ajili ya kumaliza mgogoro wa Zimbabwe.
Inaaminika mfumko wa bei kwa sasa nchini humo umepindukia asilimia 5000 hiki kikiwa ni kiwango kikubwa kabisa duniani huku wananchi wengi wakiwa hawana ajira.