Jogi Loew asema vijana wake wataimarika
30 Machi 2015Hayo ni kwa mujibu wa kocha wa timu ya taifa Joachim Loew, baada ya kipindi cha sasa cha kukifanyia majaribio kikosi chake.
Ujerumani ilitoka sare ya mabao mawili kwa mawili katika mpambano wa kirafiki dhidi ya mabingwa wa bara Asia Australia katikati ya juma lililopita kanla ya kupata ushindi wa mbili bila dhidi ya Georgia katika mchuano wa kufuzu euro 2016 jana Jumapili. Loew amesema "Ningependa kusema nimeridhishwa sana na timu yangu katika kipindi cha kwanza cha mpambano. Tulicheza vyema sana. Tumekua tukitawala. Tuliidhibiti hali. Mambo yalikuwa magumu kidogo katika kipindi cha pili. Wapinzani waliuimarisha mchezo wao, lakini bado tuliudhibiti mpira. Kulikuwa na matukio kadhaa ya hatari. Lakini licha ya hayo kitu muhimu kabisa ni kuwa tumeshinda na tumeenda nyumbani na pointi zetu".
Na wakati wakati wakiwazidi nguvu Georgia ili kusalia katika barabara ya kufuzu, Ujerumani ilikosa nafasi kadhaa za wazi huku wakionekana kukosa makali mbele ya lango la mpinzani.
Loew ambaye ameurefusha mkataba wake wa sasa hadi mwaka wa 2018, amesema anataka kuifanyia marekibisho timu iliyoshinda Kombe la Dunia ili kuiwezesha kupambana na wapinzani mbalimbali.
"timu yetu kawaida inatambulika kwa wepesi wake. Tulijaribu mifumo kadhaa tofauti ya mchezo leo. Subira ilihitajika hasa katika kipindi cha pili. Changamoto kuu ya mpinzani ilikuwa kutoutafuta sana mpira kabisa. ndio maana ulikuwa mchezo wa wasiwasi na ndio maana subira ikahitajika".
Safu ya ulinzi yenye wachezaji watatu na washambuliaji zaidi wa kutoka nyuma ni majaribio mawili ambayo ameyafanya, kando na kutafuta mchanganyiko wa chipukizi na vigogo kwenye kikosi baada ya kuondoka kwa wachezaji watatu muhimu kufuatia ushindi wa Kombe la Dunia na kurejea kwa wachezaji walioumia, wakiwemo Marco Reus, Ilkay Guendogan na Holger Badstuber. Nahodha Bastian Schweinsteiger, anasema ana furaha kubwa kurejea uwanjani.
Ujerumani, ambao wana pointi kumi pamoja na Scotland, nayo Poland ikiwa mbele yao na pointi moja katika Kundi D, watachuana na Poland Septemba 4 kabla ya kupambana na Scotland Septemba 7. Kisha watachuana na Ireland ambao wana pointi nane, mnamo Oktoba nane.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP/DPA
Mhariri: Mohammed Khelef