Jitihada za mataifa za kuisadia Somalia
16 Septemba 2013Kwa mujibu wa mkuu wa masuala ya kidiplomasia wa Umoja wa Ulaya kwa upande wa Afrika, Nicholas Westcott anasema mazungumzo hayo yanayotarajiwa kuhudhuriwa na rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud yatakuwa na mwanzo mwingine wa ujenzi wa siasa za Somalia na kujihakikishia uungwaji mkono wa jumuiya ya kimataifa.
Maeneo matano muhumu ya "Mpango Mpya"
Mpaka sasa hakuna mchango wowote uliyotangazwa na mataifa hayo ya kimataifa kabla ya mkutano huo. Mpango huo mpya utajumuisha katika kusimamia maendeleo maeneo matano muhimu katika maendeleo ya taifa hilo yakiwemo kuimarisha serikali, utawala wa sheria, usalama wa raia, kupanua wigo wa ajira na kuendeleza huduma za msingi kwa kuzingatia mapato yatakayopatikana.
Afisa huyo wa ngazi za juuu kabisa wa Umoja wa Ulaya Westcott alisema taifa la Somalia limevurugwa kabisa vita vilivyodumu kwa takribani miaka 20 kwa hivyo, wanadhamiria kujenga msingi wa taifa hilo kuanzia chini kabisa.
Al Shabab yakosoa umuhimu wa mkutano
Hata hivyo mkutano upande wa uasi umekosoa vikali mkutano huo kwa kusema "ni sawa na kupoteza muda tu" Katika taarifa yake iliyosambazwa na mtandao wa al-Shabab limesema fedha nyingi ziliwahi kutolewa kwa ajili ya Somalia hazikuzaa matunda yeyote kutokana na kunufaisha watu wachache kutokana na vitendo vya rushwa.
Kiasi ya wajumbe 50 kutoka Afrika, Ulaya, mataifa ya ghuba ya Uarabuni na kwengineko wanamatarajio makubwa na mkutano huo wa mpango mpya wa kuisaidia Somalia ambao pamoja na rais wa taifa hilo unawakutanisha, viongozi wengine wa Somalia, mashirika ya kimatiafa ya kutoa misaada na taasisi za kifedha za kimataifa.
Lakini al Shabab ambao wanapigana kuindoa madarakani serikali inayoungwa mkono na mataifa ya magharibi, wanasema mikutano kama hiyo kamwe haijawahi kuleta tija katika kuleta maendeleo katika ardhi ya Somalia na huo wa sasa utakuwa hivyo hivyo.
Somalia inapaswa kusaidiwa
Alexander Rondos Mjumbe wa Maalum wa Umoja wa Ulaya katika Pembe ya Afrika amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja uliyopita raia wa Somalia wameendelea kushuhudia mafanikio ya utendaji wa kazi wa rais, serikali na bunge, wakati mtando wa al Shabab ukiendelea kuangamizwa.
Rondos, aliendelea kusema hatua hiyo si ya kuachiwa njiani, inapaswa kuendelezwa na hasa katika kustawisha siasa za taifa hilo pamoja na usalama kwa jumla, ambazo kwa kiasi kikubwa zipo mbali na hatua ambayo inaweza kuelezwa kuwa madhubuti.
Uharamia bado umeendelea kuwa changamoto, sambamba na kundi la al Shabab ingawa kwa hivi sasa linatajwa kuwa kuwa maeneo ya kati na kusini mwa Somalia ,mbali na mji mkuu Mogadishu.
Mwandishi: Sudi Mnette DPA
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman